Magufuli azindua basi ya mwendo kasi Dar
RAIS John Magufuli amewaagiza mawaziri wanaohusika na mradi wa mabasi yaendayo haraka katika Jiji la Dar es Salaam, kuhakikisha serikali inapata faida itakayotumika kutekeleza miradi mingine yenye manufaa kwa wananchi.
Akizindua Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam na miundombinu yake, Rais Magufuli amewaagiza mawaziri wake, George Simbachawene anayeshughulikia Tamisemi na Profesa Makame Mbarawa wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, wakamweleze tangu mradi huo uanze umepata faida kiasi gani. Dk Magufuli alisema kwake haamini katika biashara ya kupata hasara “ndio maana nimeagiza mawaziri waniambie kiasi gani cha faida kimepatikana.”
Alisema ikipatikana hasara sio ya serikali, bali itakuwa ni faida ya watendaji walio kwenye mradi huo. Rais alisema watu wa Dar es Salaam, wana haki ya kufahamu kama mradi huo ni bomu au unatengeneza faida.
Aliagiza kama kuna faida ambayo imepatikana kutokana na mradi huo, ni vyema waendeshaji wa mradi wakajenga kituo cha kuegesha magari madogo katika eneo la Kimara ili kuwapa fursa wananchi, ambao wanatoka na magari nyumbani wayaegeshe hapo na kisha wapande mabasi ya mwendo kasi.
“Pale Kimara tuna eneo kubwa la barabara, jengeni pia kituo cha kuegesha daladala ambayo yatakuwa yanawabeba wananchi wanaotumia mabasi ya mwendo kasi kwa ajili ya kuwapeleka maeneo wanakoishi.
Alisema faida itakayopatikana ni lazima ijenge miradi mingine sehemu nyingine kwani deni hilo litalipwa na Watanzania wote bila kujali rangi na vyama vyao.
Aliwaonya watendaji wa DART kuhakikisha kwamba wanaachana na kujiundia vikampuni vidogo vidogo ndani ya wakala huo, kwani kufanya hivyo ni kukiuka taratibu za kazi.
Awapa rungu trafiki
Rais Magufuli pia aliagiza Kikosi cha Usalama Barabarani, kuhakikisha kinayakamata magari, pikipiki au bajaji zinazoegeshwa au kutumia barabara maalumu ya mabasi yaendayo haraka na kisha kutoa matairi yote ya vyombo hivyo vya moto, maana wana lengo la kuvuruga mradi huo.
Alisema askari wasitumie tu sheria katika kuwapa adhabu wavunjaji wa sheria hiyo, bali watumie nguvu za ziada katika kushughulikia watu wote ambao wanalenga kuvuruga mradi huo kwa kuegesha vyombo vyao vya moto kwenye barabara maalumu za mabasi hayo.
“Nawaagiza askari wakamate pikipiki, magari au bajaj pelekeni kituoni na huko toeni matairi yote, ili mwenye chombo akija akiuliza, mwambieni hamkupewa kazi ya kulinda matairi ya gari lake...hakuna wa kuwauliza mimi ndiyo Amiri Jeshi Mkuu,” aliagiza Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisema kwa kufanya hivyo, watu ambao wamezoea kuvunja sheria, wataogopa kuvuruga mradi huo ambao ni mradi wa kipekee, hivyo lazima serikali na wananchi wote wausimamie vizuri ili mataifa mengine waje kujifunza nchini namna ya kuendesha mradi huo.
Awaonya watendaji wa DART
Pia aliwaagiza waendeshaji wa mradi huo, kuhakikisha abiria hawakai muda mrefu vituoni na akaahidi kwamba kuna siku atavamia kwa kuyapanda magari hayo, hata kama atakuwa amevaa kanzu.
Alisema mradi ujikite kutatua changamoto za usafiri jijini Dar es Salaam na sio vinginevyo, kwani amedhamiria kuifanya Dar es Salaam kuwa jiji la biashara kwelikweli. Rais pia aliwaonya watendaji katika mradi huo wa DART, kuacha mara moja kujiundia vikampuni vidogo ndani ya wakala huo.
“Ninazo taarifa kwamba mnajiundia kampuni ndogo ndogo…mara kampuni ya kukatisha tiketi, mara kampuni ya ajira, mara kampuni ya mafuta...acheni mara moja,” aliagiza.
Akizungumzia mkopo wa Benki ya Dunia, Rais alisema atahakikisha kila mkopo unaotolewa na washirika wa maendeleo, unatumika kikamilifu kwa manufaa ya wananchi wote.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema baada ya mradi huo wenye kilometa 20.9 kukamilika, serikali imepanga kuanza ujenzi wa awamu ya pili ambao utahusisha Barabara ya Kilwa kutoka Mbagala Rangi Tatu hadi Posta.
Alisema kiasi cha Sh bilioni 403 zimetumika katika ujenzi wa barabara ya mabasi ya haraka awamu ya kwanza na serikali ikiwa imetoa Sh bilioni 86.5 na Benki ya Dunia imetoa Sh bilioni 317. Ujenzi wa awamu ya pili utagharimiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Post a Comment