Header Ads

MAMBO mapya yamejitokeza wakati wa shughuli ya kuaga mwili wa Stella Ibrahimu (39)


Image result for picha ya jeneza

MAMBO mapya yamejitokeza wakati wa shughuli ya kuaga mwili wa Stella Ibrahimu (39), mkazi wa Mtaa wa Mageuzi katika Manispaa ya Shinyanga aliyekufa baada ya kupigwa na mumewe Ibrahim Daniel (42).

Ibrahim alimpiga mkewe huyo kwa kosa la kutompikia mboga yenye kiwango na kutohifadhi kachumbari yake iliyowekwa kipolo kwa siku mbili. Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, Mhashamu Liberatus Sangu aliangua kilio hadharani akieleza kusikitishwa na tukio hilo ambalo amesema pamoja na kuwa ni la kusikitisha lakini pia ni tukio la aibu.

Akizungumzia tukio hilo jana, Askofu Sangu alikemea tabia ya baadhi ya wanaume kuwafanyia ukatili wanawake kwa kuwapiga vibaya na kuwasababishia vifo au ulemavu. Akihubiri katika Ibada iliyofanyika kwenye Kanisa Katoliki la Mama Mwenye Huruma lililopo Kata ya Ndembezi wakati wa kuuga mwili wa marehemu Stella ambapo alisema tukio hilo lisijitokeze tena katika familia na katika jamii.

“Narudia tena kwa kusema kuwa tukio hili sijapendezwa nalo hata kidogo, naomba lisijitokeze tena kamwe katika familia na katika jamii yetu kwani ni jambo la aibu,” alisema Askofu Sangu.

Kwa upande wake Msemaji wa familia Baraka Majigwa ambaye ni binamu wa marehemu aliwataka kina baba na kina mama wajifunze kuhusiana na tukio hilo la ukatili wa kinyama.

Pia aliwataka wanawake waache kukaa kimya kama alivyokaa kimya Stella, ambaye alikuwa akipigwa na mume wake kwa muda mrefu bila kupaza sauti. Majigwa akizungumza huku akitoa machozi kwenye umati uliofurika kwa ajili ya kumuuga marehemu alisema kina mama wameona tukio lililotendeka hivyo wanapofanyiwa ukatili wapaze sauti zao.

“Tukio hili limeniumiza mimi kwani huyu aliyefariki ni binamu yangu. Matukio kama haya yasijitokeze tena, nawaomba wakina mama pazeni sauti zenu msibaki mnateseka mpaka mnauawa kama wanyama,” alisema Majigwa.

Alisema marehemu alianza kufanyiwa ukatili miaka mingi lakini alikaa kimya na kuvumilia mateso.

Akielezea moja ya manyanyaso aliyoyapata alisema ni pamoja na tukio la kununua kiwanja kwa pesa yake lakini baada ya kumtaarifu mumewe, siku chache baadaye mumewe huyo alikiuza kimya kimya.

Alisema marehemu baada ya kusikia kiwanja chake kimeuzwa, aliwasiliana na ndugu zake ambao walimsaidia fedha na kumwezesha kukikomboa tena na baadaye alijenga nyumba kwa nguvu zake mwenyewe kwa kujishughulisha na ushonaji wa nguo na kufanya biashara ndogo ndogo.

Majigwa alieleza kuwa baada ya kumaliza kujenga nyumba hiyo alianza kuishi na mume wake na kumtimizia mahitaji mbalimbali anayoyahitaji, lakini kwa maelezo ya majirani aliishi miaka yote akimfanyia ukatili wa kumpiga mara kwa mara hadi alipofariki dunia akitetea ndoa yake.

Alisema nyumba hiyo itabaki kuwa mikononi mwa ndugu wa marehemu mpaka pale mtoto wake Daniel mwenye miaka (12) atakapojitegemea ndipo atakabidhiwa.

Aidha alisema marehemu alifunga ndoa na marehemu katika Kanisa Katoliki Ngokolo lilipo Manispaa ya Shinyanga.

Mwenyekiti wa mtaa wa Mageuzi Kata ya Ngokolo Emmanuel Sama alisema tukio hilo ni la kusikitisha na linatakiwa kukemewa lisiendelee kujitokeza tena.

Mwenyekiti wa mtaa wa Dome Kata ya Ndembezi Solomon Najulwa alisema tukio hilo si la kwanza katika mtaa wa Mageuzi kwani kuna tukio jingine kama hilo liliwahi kutokea, hivyo jamii inatakiwa kukaa katika maombi ili matukio kama hayo yasiendelee kujitokeza.

“Kina baba ambao mnawanyanyasa wanawake ni marufuku kuanzia leo kwani hii ni aibu kubwa kwetu sisi wanaume tumebadilika tumekuwa na roho za wanyama na huku Mungu alituumba na roho za upendo uvumilivu muache kwanza ni chukizo kwa Mungu,” alisema Najulwa.

Pia alisema familia hiyo ilikuwa inakaa na mtoto Elizaberth ambaye aliokotwa kwenye dampo la taka na marehemu wakati akiishi mtaa wa Dome.

Alisema baada ya kumuokota mtoto huyo marehemu alimfikisha katika ofisi ya Mwenyekiti na alikabidhiwa kuishi naye.

Alisema baada ya kukabidhiwa mtoto huyo alikuwa anaishi naye kwa upendo kama mwanaye lakini kwa vile sasa amefariki dunia, ndugu wa marehemu watakaomchukua wamlee kama alivyokuwa akilelewa na marehemu Stella.


No comments