sababu sinazo fanya wanaume kuachwa nawa penziwao
Ni matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko poa. Karibu kwenye uwanja wetu huu mzuri, tujadiliane, kuelimishana na kubadilishana mawazo kuhusu mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano wa kimapenzi. |
Wiki iliyopita, tulianza kujadili mada hii. Nikiri kwamba pengine mada hii ndiyo iliyoweka rekodi kwa mwaka huu mpya kwa kuwa na wachangiaji wengi zaidi, hasa wanawake ambao wengi walisimulia jinsi wanavyoteseka kwa kufanyiwa fujo, kutishiwa maisha na kutukanwa na wanaume ambao wameamua kuwaacha kwa sababu moja au nyingine.
Bado majibu ya kwa nini wanaume wanakuwa hivyo, hayajapatikana moja kwa moja ingawa kuna baadhi ya wasomaji wamejaribu kufafanua vizuri. Wengi wamekubaliana na mimi kwamba sababu kubwa inayofanya wanaume wasikubali kuachwa kirahisi, ni hulka yao.
Wanaamini wao ni viumbe wenye nguvu, wanaoweza kupata chochote wanachokitaka hata ikibidi kutumia nguvu. Hawaamini kwamba wanaweza kushindwa jambo hasa na watu wa jinsia ya pili (wanawake).
Wengi wanachukulia kwamba mwanaume kuachwa na mkewe au mpenzi wake ni ishara ya udhaifu mkubwa na hivyo wanajitahidi kupambana mpaka tone la mwisho.
Jambo lingine ambalo wasomaji wengi wamechangia ni kwamba Waafrika tuna mila na desturi zetu kwamba mara nyingi mwanaume ndiye anayemfuata mwanamke na kumtongoza, wakikubaliana ndiyo waanzishe uhusiano wa kimapenzi.
Kwa tafsiri hiyo, wanaume wengi huamini kwamba wao ndiyo wanaopaswa pia kuvunja uhusiano kwa sababu hatua za mwanzo, wao ndiyo waliowatongoza wale wanaowapenda, jambo ambalo kimsingi halina mantiki yoyote.
Kingine ni suala la wivu, mwanaume akishakuwa na mwanamke katika uhusiano, hataki kabisa mwanaume mwingine aje aone au afaidi yale aliyokuwa anapewa yeye. Na ikitokea akagundua kwamba mwanamke wake anatoka na mwanaume mwingine, hujenga chuki na mwanaume huyo, kiasi cha wengine kufikia hatua mbaya za kuumizana au kuuana kabisa, chanzo kikiwa ni wivu wa mapenzi.
NINI CHA KUFANYA?
Lazima tukubaliane kwamba kuna wakati mapenzi huwa yanafika mwisho, japokuwa hakuna anayependa kuona akitengana na mtu aliyempenda. Hata wanawake nao siyo kwamba hufurahia kutengana na wanaume ambao wameishi nao, wamezoeana au pengine tayari wamezaa watoto pamoja lakini kuna wakati huwa inabidi kutengana, hasa kama tatizo moja limekuwa likijirudia mara kwa mara.
Jambo la msingi ambalo wanandoa au wapenzi wanapaswa kulizingatia kabla ya kuachana ni kuhakikisha mnakaa chini na kuzungumza, kila mmoja aeleze hisia zake. Utashangaa kwamba wanandoa hata kama walikuwa wamekoseana mambo makubwa kiasi gani, wanapokaa mara ya mwisho kwa ajili ya kukubaliana kuachana, hufikia muafaka na kufungua ukurasa mpya.
Lakini kama hilo nalo limeshindikana, kubalianeni kwa amani. Mwisho wa mapenzi haumaanishi mwanzo wa wa chuki kati yenu. Wanachokosea wengi ni kwamba hutaka kuachana kwa vurugu, kutukanana, kutoleana kashfa na vitu vya namna hiyo.
Kama mnaona mmeshindwana kabisa, kubalianeni kuachana kwa amani, endeleeni kuheshimiana na kila mmoja aanzishe maisha yake. Ukiona mnashindwa kukubaliana kuhusu hilo, basi uwezekano mkubwa ni kwamba bado mnapendana na pengine mnapaswa kufikiria suluhu kuliko kutengana.
Ukweli ambao huwezi kuupinga ni kwamba ukiona watu wameachana lakini bado wanafuatiliana, wanafanyiana fujo au kutoleana kashfa, bado wanapendana isipokuwa tatizo ni kwamba hakuna anayekubali kujifanya mjinga na kujishusha ili kuokoa penzi linalozama.
Hata kama wewe ni mwanaume na una nguvu kiasi gani, neno ‘samahani’ ni dogo lakini lina nguvu kubwa ya kuweza kubadilisha kabisa mawazo ya mwenzi wako, hasa kama anayelitoa neno hilo anamaanisha kutoka ndani ya moyo wake.
Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine.
Post a Comment