Mwanasoka maarufu nchini Kenya, Joe Kadenge, amelazwa katika hospitali moja mjini Nairobi baada ya kuugua.
Nyota huyo mstaafu aliyeiwakilisha klabu ya Afc Leopards na timu ya taifa ya Kenya, alikimbizwa hospitalini mapema wiki hii baada ya kuugua kisukari.
Wachezaji wenzake wa zamani, George Sunguti na Reginald Asibwa walimsaidia kumfikisha hospitalini baada ya kuzidiwa na maumivu.
Hata hivyo familia yake inasema kuwa Kadenge amepata nafuu na hali yake inaendelea kuimarika.
Ni mara ya pili shujaa huyo kuugua na kukimbizwa hospitalini .
Mwezi Oktoba, Kadenge alikimbizwa hadi hospitali ya Meridian mjini Nairobi alipokuwa akitazama mechi ya ligi ya soka ya taifa hilo.
"Amepata nafuu kwa sasa na mke wake amejiunga naye hospitalini kumsaidia," Sunguti ameliambia gazeti la Nation nchini Kenya.
Wapenzi wa soka nchini humo wamekuwa wakimtakia mzee huyo nafuu.
Mnamo mwezi Septemba Kenya ilimpoteza kocha na mchezaji maarufu James Sianga aliyefariki baada ya kuugua kwa kipindi kirefu magharibi mwa Kenya.
Post a Comment