Polisi wateketeza magunia 58 ya bangi kwa moto
JESHI la Polisi mkoani Arusha kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama nchini vimefanikiwa kuteketeza kwa kuchoma moto magunia 58 ya bangi na mbegu zake kilo 210.
Mbali ya hilo, vikosi hivyo vya ulinzi vilifanikiwa kuteketeza ekari 31 za mashamba ya bangi zoezi zima lilifanyika kwa siku mbili katika wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa polisi nchini ambaye ni Mkuu wa kitengo cha Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya, Mihayo Msikhela alisema kuwa operesheni hiyo ilifanyika majira ya saa 11 alfajiri, Januari 10 hadi 12 katika wilaya ya Arumeru, kijiji cha Kisimiri Juu na kufanikiwa kuteketeza mazao hayo haramu.
Msikhela alisema operesheni hiyo ni ya nchi zima lakini wameanzia katika Mkoa wa Arusha, wilaya ya Arumeru wenye sifa kubwa ya kilimo cha bangi hapa nchini.
Alisema wilaya zinazoongoza kwa kilimo cha bangi hapa nchini ni Arumeru na Tarime na kusema kuwa watu wanaofanya biashara hiyo wanaombwa kuacha mara moja vinginevyo vyombo vya dola havitasita kuwachukulia hatua kwa kulima kilimo cha bangi.
Msikhela aliwaasa viongozi wa serikali ngazi ya kijiji na kata kuwafichua wanaofanya shughuli hiyo kwani wao ndio wanaowajuwa lakini wanawaficha kwa maslahi yao hivyo nao watachukuliwa hatua kali.
“Tunataka viongozi wa serikali wa ngazi hizo kushirikiana na polisi kuwafichuwa wahusika bila ya woga lakini hilo halifanyiki…kuna taarifa kuwa viongozi wanashiriki kuwahifadhi wakulima wa kilimo cha bangi, nao tutawatia mbaroni kwa kuwa nao ni wahalifu kwa kuficha wahalifu,” alisema.
Post a Comment