Header Ads

treni ya abiria ya Deluxe, iliyokuwa ikitoka mkoani Kigoma kwenda Dar es Salaam kuanguka mkoani Pwani.


WATU kadhaa wamejeruhiwa, mmoja akiwa ana hali mbaya baada ya mabehewa tisa ya treni ya abiria ya Deluxe, iliyokuwa ikitoka mkoani Kigoma kwenda Dar es Salaam kuanguka mkoani Pwani.
Katika mabehewa hayo, manne yameanguka, matatu yameacha njia na mawili yametenguka.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Boniventure Mushongi, mabehewa yaliyoanguka ni saba na kwamba wanaendelea kuwaokoa majeruhi.
Akizungumza kwa njia ya simu, Msemaji wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Midladjy Maez alisema ajali hiyo ilitokea saa 9:40 alasiri katika Kitongoji cha Kambini Ruvu Ngeta, Kata ya Kikongoa Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani. Maez alisema mabehewa hayo yalianguka baada ya treni kuacha njia na kusababisha majeruhi kadhaa.
“Ni kweli ajali hiyo imetokea na kusababisha majeruhi na hadi wakati huo kulikuwa hakuna taarifa yoyote ya kifo kilichotokana na ajali hiyo, licha ya kwamba mtu mmoja ndiyo hali yake mbaya,” alisema Maez, bila kutaja sababu za ajali hiyo.
“...Imeripotiwa watu kadhaa wamejeruhiwa na mmoja amejeruhiwa sana, hizi ni taarifa za awali…baada ya kikosi cha uokoaji kumaliza kazi ya kuinua mabehewa ndio taarifa ya waathirika itakamilika,” alisema Maez katika taarifa yake.
Alisema treni hiyo ilitakiwa ifike Dar es Salaam saa 11 jioni, lakini ilipofika hapo mabehewa hayo yalianguka na kusababisha kushindwa kuendelea na safari.
“Kutokana na ajili hiyo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na Mkurugenzi Mkuu wa TRL wanaelekea eneo la tukio ili kuweza kujua kilichotokea,” aliongeza msemaji huyo wa TRL.



CHANZO HABARI LEO

No comments