Header Ads

WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesisitiza kuwa suala la mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi limekwishatolewa taarifa


Image result for picha ya malawi

WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesisitiza kuwa suala la mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi limekwishatolewa taarifa na Wizara hivi karibuni na kwamba lipo chini ya Jopo la Usuluhishi linaloundwa na viongozi wastaafu wa Afrika kutoka nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Wizara hiyo imefikia hatua ya kusisitiza hilo kutokana na baadhi ya vyombo vya habari hususani magazeti kupotosha lengo la mkutano wa wizara hiyo na waandishi wa habari uliofanyika Januari 26, mwaka huu.
Katika tarehe hiyo, wizara hiyo ilikutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa taarifa kwa umma kuhusu Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi ambao umepangwa kufanyika mjini Lilongwe, Malawi Febuari 3 hadi 5, mwaka huu.
Katika taarifa ya ufafanuzi jana, Wizara hiyo ilisema; “Hata hivyo, vyombo vingi vya habari hususan Magazeti ya tarehe 27 Januari, 2017 vimeandika kwamba Mkutano huo ni maalumu kwa ajili ya kujadili mgogoro wa Mpaka kati ya Tanzania na Malawi kwenye Ziwa Nyasa pamoja na kesi ya Watanzania nane waliokamatwa kwa madai ya kuingia nchini Malawi bila kibali.
“Wizara inapenda kuchukua nafasi hii kutoa ufafanuzi kwamba, suala la mgogoro wa mpaka limekwishatolewa taarifa na Wizara hivi karibuni kwamba lipo chini ya Jopo la Usuluhishi linaloundwa na Viongozi Wastaafu. “Jopo hilo linaongozwa na Joachim Chissano, Rais Mstaafu wa Msumbiji akisaidiwa na Festus Mogae, Rais Mstaafu wa Botswana na Thabo Mbeki, Rais Mstaafu wa Afrika Kusini.
“Aidha, kuhusu suala la Watanzania wanane waliokamatwa kwa madai ya kuingia nchini Malawi bila kibali lipo Mahakamani hivyo halitakuwa sehemu ya mazungumzo ya Mkutano wa Tume ya Pamoja.
Kwa mujibu wa Wizara hiyo, mantiki ya Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati Tanzania na Malawi ni njia mojawapo ya kuendelea kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.
Imesema mkutano huo ambao ni wa kawaida, una lengo la kujadili na kutathmini hatua zilizofikiwa katika utekelezwaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika Mkutano wa Tatu wa JPCC uliofanyika nchini Juni 24 hadi 30, mwaka 2003.

No comments