RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein amezindua kiwanda cha maziwa cha kisasa
RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein amezindua kiwanda cha maziwa cha kisasa cha Kampuni ya Azam Dairy Production Limited(ADPL).
Dk. Shein alitembelea kiwanda hicho cha kisasa na kupata maelezo ya kitaalamu kutoka kwa Meneja Uzalishaji wa Kampuni ya Azam Dairy Production Limited (ADPL), Adilson Fagundes.
Katika hotuba yake, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar(SMZ) imeamua kwa makusudi kuendeleza sekta ya viwanda kwa kutambua umuhimu wake katika maendeleo ya Zanzibar, sambamba na historia yake katika sekta hiyo na sekta ya biashara.
Rais Shein alieleza kuwa serikali ipo katika hatua za mwisho za uandaaji wa sera mpya za viwanda itakayozingatia zaidi matumizi ya malighafi zinazopatikana nchini na kueleza azma ya kuunganisha viwanda na sekta ya utalii.
Rais Shein alitumia fursa hiyo kueleza azma ya Serikali ya kuanzisha kiwanda cha kusindikizia samaki hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar ni visiwa vilivyozungukwa na bahari, hivyo malighafi za kiwanda hicho ni rahisi kupatikana.
Dk. Shein aliwahakikishia wananchi kuwa mji wa Fumba utafunguka kutokana na mipango kabambe ya serikali katika kuliimarisha eneo hilo la uwekezaji kwa upande wa Unguja na Micheweni kwa upande wa Pemba.
Rais Shein alisema kuwa kiwanda hicho ni cha kisasa na mitambo yake haipo katika nchi nyingi za bara hili la Afrika na hata nje ya bara hili na kusifu hatua hiyo na kusisitiza haja kwa taasisi husika kuwashawishi wananchi kunywa maziwa kwani imegundulika wananchi wa Zanzibar si watumiaji wazuri wa maziwa.
Aidha, Dk. Shein alieleza haja ya kiwanda hicho kuweka siku moja maalum ya kitaifa ya kunywa maziwa, hatua ambayo itawahamasiha wananchi mbalimbali wa Zanzibar kunywa maziwa na kuiondoa Zanzibar kuwa ya mwisho katika unywaji wa maziwa kwa nchi za Afrika Mashariki.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Khalid Salum Mohammed alieleza kuwa sekta ya uwekezaji ina mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa nchi na ndio maana Rais Shein amekuwa akilisimamia hilo kwa nguvu zake zote na mafanikio makubwa yanaendelea kupatikana.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), Salum Khamis Nassor alieleza mikakati iliyowekwa na Serikali ya Zanzibar katika kuanzisha na kuendeleza maeneo huru huku akieleza namna Mamlaka yake ilivyoshirikiana na muwekezaji huyo kuanzisha kiwanda hicho.
Awali Mwakilishi wa Kampuni hiyo ya Azam, Salim Aziz alieleza kuwa kiwanda hicho kina mitambo ya kisasa ya kusindika maziwa ambayo husindika maziwa kwa kuyapitisha katika mfumo maalum wa joto kwa ajili ya kuyahifadhi na kuuwa wadudu na kwamba uwekezaji huo umegharimu Dola za kimarekani milioni 20.
Alisema kuwa kiwanda hicho kina uwezo wa kusindika jumla ya lita 160,000 kwa siku, ambapo kiwanda kinaweza kutumia malighafi ya maziwa safi na maziwa ya unga na kueleza changamoto iliyopo ya upatikanaji wa maziwa safi.
Post a Comment