WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza viongozi wa Idara ya Uhamiaji kuandaa semina
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza viongozi wa Idara ya Uhamiaji kuandaa semina za mafunzo ya elimu ya uraia kwa wahudumu ya hoteli na nyumba za kulala wageni nchini ili kudhibiti wimbi la wahamiaji haramu.
Alitoa kauli hiyo juzi mara baada ya kuwasili katika Ikulu ndogo ya Njombe na kupokea taarifa ya mkoa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa huo, Christopher Ole Sendeka.
Katika taarifa hiyo, Ole Sendeka alisema kwenye kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba, 2016 Idara ya Uhamiaji ilibaini kuwepo kwa raia 119 wa kigeni ndani ya mkoa huo, ambapo wahamiaji haramu 42 walikamatwa.
“Anzisheni utaratibu wa kutoa semina kwa wahudumu wa hoteli na nyumba za kulala wageni. Hawa wakipata elimu ya uraia watawasaidia katika kutoa taarifa za kuwepo kwa wageni ambao wana mashaka na uraia wao,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa mikoa kujikita katika ukusanyaji wa mapato, kuzuia mianya ya rushwa pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma katika maeneo yao.
Aliwataka pia wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia vizuri miradi ya maendeleo inayojengwa katika maeneo yao kuhakikisha kama inalingana na thamani halisi ya fedha zinazotolewa na wasikubali kupokea miradi iliyojengwa chini ya kiwango.
Awali Mkuu wa mkoa huo, alisema kati ya wahamiaji haramu 42 waliokamatwa 39 ni raia wa Ethiopia, wengine na idadi yao kwenye mabano ni wanatoka Uganda (1), Burundi (1) na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (1). Wote walifikishwa mahakamani na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Alisema Idara ya Uhamiaji inaendelea na mikakati ya kuishirikisha jamii katika utoaji wa taarifa pindi wanapowatilia shaka kuhusu ukazi wao ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya uraia na upanuzi wa huduma za uhamiaji.
Akizungumzia kuhusu suala la ukusanyaji wa mapato, Mkuu wa mkoa alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016 mkoa uliweza kukusanya Sh bilioni 7.07 sawa na asilimia 89.3 ya makisio ambayo yalikuwa shilingi bilioni 7.92.
Post a Comment