ASILIMIA 96 ya Watanzania wanakubali utendaji wa Rais John Magufuli tangu alipoingia madarakani
ASILIMIA 96 ya Watanzania wanakubali utendaji wa Rais John Magufuli tangu alipoingia madarakani Novemba mwaka jana, huku asilimia 69 wakikubaliana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano, hususan uondoaji wafanyakazi hewa huku elimu kuwa bure ikikubaliwa kwa asilimia 67 na asilimia 61 ikikubali kusimamishwa kazi kwa watumishi wa umma (kutumbuliwa kwa majipu).
Wakati asilimia 96 ya Watanzania wakikubali utendaji kazi wa Rais Magufuli tangu aingie Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam, Novemba 5, mwaka jana, asilimia 78 wanawakubali wenyeviti wa mitaa na kijiji, asilimia 74 wakikubali utendaji wa madiwani na wabunge wakiwa wa mwisho kwa kukubalika kwa asilimia 68.
Matokeo haya yametolewa na Taasisi ya Twaweza kwenye utafiti uitwao Rais wa Watu? Tathmini na matarajio ya wananchi kwa Serikali ya Awamu ya Tano.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze,
muhtasari huo unatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, ambao ni
utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia
simu za mkononi. Matokeo haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa
kutoka kwa wahojiwa 1,813 kutoka maeneo yote Tanzania Bara (Zanzibar
haihusiki kwenye matokeo haya) kati ya Juni 4 na 20, mwaka huu.
Aidha, wadau wameshauri ripoti hiyo kufanyiwa kazi zaidi, lakini pia
wakibainisha kuwa ni taarifa inayotoa taarifa kama ni yapi ya kufanyiwa
kazi zaidi kwa mustakabali wa Taifa.
Kuhusu wananchi kama wanawafahamu wawakilishi wao, Eyakuze
alibainisha kuwa asilimia 98 ya wananchi wanafahamu utendaji wa Rais
wao, asilimia 96 ikiwa ni kufahamu ofisa mtendaji wa kijiji, asilimia 92
kwa diwani na mbunge na asilimia 21 kwa mkurugenzi mtendaji wa wilaya.
Kuhusu wananchi kuwa na taarifa kiasi gani katika masuala ya siasa,
alisema asilimia 61 ya wananchi hawana taarifa huku wenye nazo wakiwa ni
asilimia nne tu.
Alisema wananchi waliohojiwa walisema (kwa nyakati tofauti) kuwa wana
uzoefu wa kukutana na watendaji wa ngazi kama vile ofisa mtendaji
lakini wachache wakiwa wanakutana na wabunge wa majimbo yao.
“Pale ambapo wananchi wameongea na viongozi wao, asilimia kubwa
walizungumzia masuala ya kijamii badala ya masuala binafsi ama ya
kitaifa,” alisema Eyakuze na kuongeza kuwa mara nyingi kukutana huko
hutokea kwenye mikutano ya umma, majumbani au maofisini mwa viongozi wa
ngazi ya kijiji na kata.
Mtendaji huyo alisema wananchi wengi wanasema Serikali ya Awamu ya
Tano imeleta maboresho kwenye huduma nyingi za umma ikiongozwa na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuboresha huduma zake, huduma kuwa
nzuri shuleni, vituo vya Polisi, mahakamani, vituo vya afya na mamlaka
za maji.
Alisisitiza kuwa takwimu hizo zinaonesha mitazamo na maoni ya
wananchi kuhusu huduma za umma na siyo lazima ikawa ndiyo hali halisi ya
mabadiliko kwenye huduma hizo.
Akiizungumzia ripoti hiyo, Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya
Serikali (TSN), wachapishaji wa magazeti ya Daily News, HabariLeo,
Sunday News, HabariLeo Jumapili na SpotiLeo, Dk Jim Yonaz alisema
taarifa hiyo inaonesha kuwa wananchi hawana jambo wanalosema ni baya.
Alisema ripoti inatoa taarifa kwamba ni yapi ya kufanyiwa kazi na
inatoa fursa kwa watendaji waliochaguliwa na Rais Magufuli kuhakikisha
wanakubalika kama yeye mwenyewe alivyokubalika kulingana na ripoti.
Post a Comment