Header Ads

Wadau wanaichukulia kama TFF inaionea Azam FC kwa kuinyima haki ya kutumia kiwanja chake cha nyumbani





MJADALA mkubwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusU mambo ya michezo kwa wiki nzima sasa, imekuwa ni wapi ichezwe mechi kati ya Azam FC na Simba. Kumekuwa na kurushiana maneno kutoka pande mbili ambazo zimejigawa aidha kuisaidia Azam FC au Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa upande mwingine.
TFF inaonekana kwa namna moja au nyingine kuzikingia kifua klabu za Simba na Yanga kutocheza mechi zao kwenye kiwanja cha nyumbani cha Azam ambacho ni Chamazi Complex, huku kukiwa na mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zikiwahi kupigwa katika dimba la Chamazi.
Mechi za ligi kwa miaka minane tangu Azam iingie Ligi Kuu hazichezwi uwanjani kwani nikimaanisha zile wanazocheza ama na Simba au Yanga na hata kama wakipanga mechi ya kirafiki ni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wadau wanaichukulia kama TFF inaionea Azam FC kwa kuinyima haki ya kutumia kiwanja chake cha nyumbani kwenye mechi za Simba na Yanga na hivyo kuonekana kama wanazibeba timu hizo dhidi ya Azam na kuonekana ni hujuma. Jambo hili limepata msukumo mkubwa kipindi hiki cha msimu huu hasa baada ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF ambaye sasa ni Mtendaji Mkuu wa Azam FC Saad Kawemba kuwepo Azam.
Kawemba alikuwa Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF kipindi cha utawala wa Leodegar Tenga, lakini alipoingia Jamal Malinzi na timu yake akawekwa kando. Ikumbukwe kwamba Azam FC haikuanza leo kupigania kutumia Uwanja wa Chamazi Complex dhidi ya Simba na Yanga. Tangu Kawemba akiwa TFF, Azam FC ilikuwa kwenye hii vita.
Katika moja ya matukio ya kushangaza kabisa ni pale TFF ya Tenga ambayo Kawemba akiwa Mkurugenzi wa Mashindano ilipohamisha mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar kutoka Chamazi na kuletwa Uwanja wa Taifa na Azam ilipoteza kwa mabao 2-1.
Mechi hii awali ilichezwa Chamazi na Mtibwa kugomea penalti ya dakika za majeruhi ambayo Azam iliipata kutokana na mchezaji mmoja wa Mtibwa kushika mpira kwenye eneo la hatari. Mwamuzi akaamuru penalti ambayo Mtibwa waligomea na mchezo kumalizikia hapo. Kanuni za Ligi Kuu ziko wazi juu ya mchezo kuvunjika kwa namna ile.
Ni Wazi Mtibwa walistahiki kupoteza mchezo kwa kitendo chao cha kugomea, lakini ajabu ni pale TFF walipoamua mechi irejewe Uwanja wa Taifa.
Kama marejeo yalikuwa ni matakwa ya kikanuni, kwa nini haikurejewa Chamazi? Ikimbukwe wakati ule Azam FC walikuwa wakiikimbiza Simba hii hii kwenye ubingwa, kama Azam ingeshinda ile mechi ilikuwa inajiwekea mazingira mazuri.
Lakini wakubwa wa TFF waliona busara ni kuileta mechi Taifa, ambako Azam walipigwa 2-1 na kuipalilia Simba ubingwa.
Hapa nilikuwa najaribu kuonesha pande mbili za Kawemba juu ya suala la matumizi ya Uwanja wa Chamazi kwa Azam FC, ambapo akiwa TFF aliona bora Taifa kuliko Chamazi na wala hakusikika hata siku moja kuitakia Azam icheze Chamazi, leo hayupo TFF yupo Azam anazungumzia la haki yao. Je, leo akirudi kuwa Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF atayasema haya anayoyasema leo kwa kinywa kipana kuitetea Azam FC?

No comments