Header Ads

LIGI Kuu Tanzania bara inaendelea tena leo





LIGI Kuu Tanzania bara inaendelea tena leo ambapo wababe watatu Simba, Azam na Yanga zitawania pointi tatu muhimu. Aidha, ndugu wawili katika mkoa mmoja, Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.
Wakati Simba na Azam FC zikitarajiwa kucheza leo kwenye Uwanja wa Uhuru, Yanga itakuwa kwenye uwanja wa Kambarage Shinyanga kumenyana na Mwadui FC.
Mechi itakayoteka hisia za mashabiki wa soka ni Simba dhidi ya Azam FC kutokana na timu hizo kuwa na upinzani mkali zinapokutana lakini hasa katika kipindi hiki ambapo zimelingana kila kitu kwenye msimamo zikiwa na pointi 10.
Simba imeshacheza michezo minne na kushinda mitatu dhidi ya Ndanda FC mabao 3-0, dhidi ya Mtibwa Sugar mabao 2-0, dhidi ya Ruvu Shooting mabao 2-1 na kupata sare ya bila kufungana dhidi JKT Ruvu.
Matokeo hayo ni sawa na Azam iliyoshinda michezo mitatu dhidi ya Mbeya City mabao 2-1, dhidi ya Tanzania Prisons bao 1-0, dhidi ya Majimaji mabao 3-0 na kupata sare moja dhidi ya African Lyon bao 1-1.
Timu hizi mara nyingi zinapokutana hutoka sare hakuna aliyemuonesha mwenzake ubabe. Msimu uliopita mchezo wa kwanza zilipata sare ya mabao 2-2 na pia, ziliwahi kupata sare ya bila kufungana.
Wachezaji ambao wamekuwa wakifunga pindi timu hizi zinapokutana ni John Bocco na Ibrahim Ajib. Bado wote wapo msimu huu na wataendelea kutazamwa kama wataendeleza ubabe wao.
Mechi hii huenda ikawa ngumu na pengine kukawa na mabao kutokana na kila mmoja kuonesha ubora kutokana na aina ya wachezaji ilionao na makocha wapya lakini pia, kila mmoja anataka kukaa kileleni.
Uhondo wote utajulikana leo. Katika uwanja wa Kambarage Yanga itacheza na Mwadui FC. Mchezo wa msimu uliopita ugenini, timu hiyo ya Jangwani ililazimishwa sare ya mabao 2-2.
Yanga imeshacheza michezo mitatu ikishinda miwili dhidi ya Majimaji mabao 3-0, dhidi ya African Lyon mabao 3-0 na kupata sare moja dhidi ya Ndanda FC 0-0 na hivyo, kufikisha pointi saba.
Mwadui FC imeshinda mchezo mmoja dhidi ya Mbao FC bao 1-0 na kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Stand United, ikifungwa dhidi ya Toto African bao 1-0 na dhidi ya Kagera Sugar bao 1-0 hivyo, kufikisha pointi nne.
Kila timu inahitaji matokeo. Huenda ikawa mechi ngumu kwani Yanga inahitaji matokeo mazuri kujihakikishia nafasi ya kutetea ubingwa wake na Mwadui FC ikitaka pia kufanya vizuri kujiweka pazuri.
Jijini Mbeya kutakuwa na mchezo wa ndugu wawili, Mbeya City ikiwa mwenyeji wa Prisons kwenye uwanja wa Sokoine. Msimu uliopita Prisons ilikuwa mbabe baada ya raundi ya kwanza kutoka sare ya bila kufungana na raundi ya pili kushinda bao 1-0.
Huenda Mbeya City iliyoanza vizuri msimu huu ikalipiza kisasi. Pia, mechi nyingine itakuwa ni kati ya Mtibwa Sugar dhidi ya Kagera Sugar kwenye uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro. Itakuwa mechi yenye upinzani kutokana na kuwa na makocha wawili waliowahi kuichezea Mtibwa Sugar.
Salum Mayanga anayeifundisha Mtibwa na Mecky Mexime wa Kagera Sugar, wote wakiwa wamewahi kucheza Mtibwa Sugar kwa nyakati tofauti.

No comments