WABUNGE wote wa Chama cha Wananchi (CUF) wametangaza rasmi kutomtambua aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
WABUNGE wote wa Chama cha Wananchi (CUF) wametangaza rasmi
kutomtambua aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim
Lipumba.
Wamemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi
kutomkumbatia mwanasiasa huyo aliyebobea katika uchumi, ikielezwa kwa
sasa hana sifa za kuwa mwenyekiti wa chama hicho, labda aanze upya
mchakato.
Wameeleza msimamo huo jana mjini Dodoma na Mbunge wa Viti Maalumu,
Riziki Mngwali ambaye pia ni Kiongozi wa Wabunge wa CUF katika mkutano
baina ya waandishi wa habari za Bunge na wabunge wa CUF isipokuwa Mbunge
wa Jimbo la Kaliua, Magdalena Sakaya aliyesimamishwa uanachama, ingawa
anaendelea kutimiza majukumu yake bungeni.
Mngwali alisema Profesa Lipumba amekuwa akijaribu kukiyumbisha chama
na hivi karibuni kudai amekaririwa akisema anasubiri barua ya Msajili wa
Vyama vya Siasa ya kuthibitishiwa kuendelea na uenyekiti wake.
“Wakati anajiuzulu uenyekiti Agosti 5, mwaka jana aliutangazia umma
na kudai anakwenda Rwanda kwa kazi aliyodai ya utafiti ili aje kuisaidia
serikali, lakini inashangaza sasa anataka kujirejeshea uenyekiti. Hilo
hatukubali kwa kuwa chama kina taratibu zake,” alisema.
Aliongeza kuwa, alikiacha chama katika wakati mgumu kuelekea Uchaguzi
Mkuu, lakini kikaimarika zaidi kwa kupata wabunge 43, madiwani 287,
kuongoza manispaa mbili na halmashauri za wilaya tatu, hivyo
wanashangazwa kuona akitaka kurejea, tena kwa kutumia nguvu.
“Tunataka ifahamike kwa dhati kuwa, sisi wabunge, hatumtambui tena
Profesa Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF,” alisema Mngwali na kumtaka
Msajili kutomuidhinisha Lipumba, kitendo alichodai kitachochea mgogoro
ndani ya chama.
Aliongeza kuwa badala ya kutumia mabavu kutaka kurejea madarakani, ni
vyema akabaki na heshima yake, kwani amekitendea mambo mengi chama
hicho na kwamba wanamheshimu, hivyo afuate taratibu za kichama kutaka
kuwania tena uenyekiti.
Mngwali alisema wamekubaliana na uamuzi wa Baraza Kuu la Uongozi wa
CUF wa kuwasimamisha uanachama Lipumba na wenzake tangu Agosti 28, 2016
kutokana na kile kinachodaiwa kukiuka Katiba ya chama hicho. Miongoni
mwa tuhuma zao ni kusababisha vurugu wakati wa Mkutano Mkuu Maalumu wa
Uchaguzi Agosti 21, mwaka huu jijini Dar es Salaam uliokuwa unalenga
kumthibitisha Juma Duni Haji kuwa Mwenyekiti mpya.
Hata hivyo, kutokana na vurugu zilizoibuka, mkutano huo ulivunjika.
Mbali ya Lipumba na Sakaya, wengine waliositishiwa uanachama ni Abdul
Kambaya ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho,
Ashura Mustapha, Omar Mhina, Thomas Malima, Kapasha M. Kapasha, Mohamed
Habib Mnyaa, Haroub Shamis na Mussa Haji Kombo.
Ashura ni mjumbe wa Baraza Kuu na aliwahi kuwa Naibu Mkurugenzi wa
Habari na Mawasiliano ya Umma CUF wakati Mnyaa na Kombo, walikuwa
wabunge kipindi cha 2010/2015, Mnyaa akiwakilisha Jimbo la Mkanyageni na
Kombo Jimbo la Chake Chake, kisiwani Pemba.
Kutokana na kusimamishwa kwa viongozi hao, Naibu Katibu Mkuu
Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alimtangaza Julius Mtatiro aliyewahi kuwa
Naibu Katibu Mkuu Bara kuwa kiongozi wa Kamati ya Uongozi wa muda
inayowajumuisha pia wabunge Katani Ahmed Katani na Savelina Mwijage
ambao ni wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
Post a Comment