MAAFA zaidi yameripotiwa katika janga la tetemeko la ardhi, lililotokea juzi mkoani Kagera
MAAFA zaidi yameripotiwa katika janga la tetemeko la ardhi,
lililotokea juzi mkoani Kagera, ambapo imeripotiwa idadi ya vifo
kuongezeka na kufikia watu 16, huku wengine 253 wakijeruhiwa na
kusababisha simanzi na masikitiko kwa familia nyingi. Katika tukio hilo,
pia nyumba 840 za makazi zimeanguka, nyumba 1,264 zimepata nyufa kubwa
na majengo 44 ya taasisi mbalimbali zikiwemo shule yameanguka.
Tukio hilo limemfanya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kulazimika kufanya
ziara ya ghafla ya kuwatembelea waathirika wa tetemeko hilo, ambalo
limedaiwa kusababisha tafrani pia katika nchi jirani za ukanda wa Afrika
Mashariki za Kenya na Rwanda.
Katika hatua nyingine, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha
Nelson Mandela kilichopo eneo la Tengeru, mkoani Arusha kimeeleza mpango
wa kuanza kufunga vifaa vitakavyotoa ishara ya matukio ya matetemeko ya
ardhi kabla majanga hayo kutokea.
Katika mradi huo maalumu chini ya Kitengo cha Utafiti wa Miamba na
Volcano, chuo hicho kitashirikiana na taasisi mbalimbali za elimu ya juu
zilizopo Ulaya na Marekani, hasa Chuo Kikuu cha Glasgow kilichopo
Scotland, kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa taasisi hiyo, Profesa Burton
Mwamila. Ziara ya Waziri Mkuu
Akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu jana katika Uwanja wa Kaitaba ulioko
mjini Bukoba ambapo umeandaliwa maalumu kwa ajili ya kuaga miili ya watu
waliopoteza maisha katika tukio hilo la kusikitisha, Mkuu wa Mkoa, Meja
Jenerali mstaafu Salum Kijuu alisema tukio hilo ni la kwanza kutokea
mkoani humo na kwamba limeleta madhara makubwa kwa wananchi na kuacha
majonzi makubwa.
Kijuu alisema mpaka taarifa inaandaliwa watu 16 waliripotiwa kupoteza
maisha na kusababisha majeruhi 253, huku 170 wakiwa wamelazwa katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo na 83 wakitibiwa na kuruhusiwa.
Alisema pia tetemeko hilo limesababisha nyumba 840 za makazi
kuanguka, nyumba 1,264 kupata nyufa kubwa na majengo 44 ya taasisi
mbalimbali zikiwemo shule kuanguka.
Alisema tetemeko hilo lenye ukubwa wa alama 5.7 uliopimwa kwa kipimo
cha Ritcher cha kisayansi cha kupima matetemeko, limeleta madhara
makubwa ambapo Serikali ya Mkoa inaendelea kutathmini kwa kina athari
zaidi zilizosababishwa na tetemeko hilo na pia uharibifu uliojitokeza
kisha kupeleka katika Ofisi ya Waziri Mkuu waone jinsi ya kusaidia.
Alisema hatua zilizochukuliwa na mkoa mpaka sasa ni kuwaokoa na
kuwapeleka watu hospitali kwa ajili ya matibabu na kuwapatia makazi ya
muda baadhi ya wananchi wenye nyumba zilizoathirika, wakati mipango
mingine ikiandaliwa.
Taarifa hiyo ya Mkuu wa Mkoa, ilimfanya Waziri Mkuu kueleza
masikitiko yake na serikali kutokana na janga hilo na kutoa salamu za
pole kwa wananchi waliopatwa na madhara na kuwatembelea wagonjwa
waliolazwa katika Hospitali ya Mkoa na pia maeneo yote yaliyoathirika.
"Leo si siku nzuri kwetu, nimekuja kumwakilisha Rais wetu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ambaye anawapa pole sana wana Kagera wote na
Watanzania kwa ujumla. Pia Makamu wa Rais anawapa pole kwa msiba huu
mkubwa, lengo la safari yangu ni kuja kuwapa pole, tukio hili ni kubwa
na halijawahi kutokea Tanzania, tumekuwa tukisikia kutoka mataifa ya nje
lakini leo limetupata nchini kwetu," alisema Majaliwa.
Aliwasihi na kuwataka wananchi kuwa wavumilivu, kuonesha umoja na
ushirikiano, lakini pia kujitokeza kuwafariji wenzao wakati wote wa
majonzi, huku akisema Watanzania kwa miaka mingi wamekuwa wakishuhudia
mitikisiko midogo, lakini juzi tumeshuhudia mtikisiko mkubwa kabisa
ambao umeleta madhara makubwa kwetu.
"Mpaka sasa hatuna uhakika mtikisiko huu utakuwa endelevu kwa kiasi
gani, nataka niwahakikishie Watanzania wote, Serikali tunafanya
mawasiliano na taasisi zenye uwezo wa kubaini mtikisiko huu ili tuweze
kujua jambo hili litakuwa endelevu kwa kiasi gani na kuona dalili na
ukubwa wake utakuwaje ili tujipange katika kutoa elimu lakini pia
tahadhari pindi jambo kama hili linapoweza kutokea au tunapoona
viashiria au dalili za jambo hili," alisema Waziri Mkuu.
Alisema kuwa Mkuu wa Mkoa katika taarifa yake alimweleza kwamba
tathmini inaendelea na kwamba ameiagiza Kamati ya Maafa ya Ofisi ya
Waziri Mkuu kufika mkoani Kagera mara moja na kuzunguka mkoa mzima kwa
kushirikiana na uongozi wa mkoa kwa lengo la kufanya tathmini ya jumla.
Alisema baada ya tathmini hiyo, utaratibu utafuatwa kwani serikali
haiwezi kuwatupa mkono wananchi hao, pia alitumia fursa hiyo kuwaambia
wafiwa kuwa Watanzania nchini kote wako pamoja nao katika janga hilo.
Akielezea mkasa huo, majeruhi Happines Apolinary ambaye ni mkazi wa
kata ya Buyekera aliyelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera kwa
kuumia kichwani na mgongoni, alisema alishtuka kusikia mtikisiko mkubwa
wakati akiwa ndani ya nyumba yake na ghafla aliangukiwa na kuta na
kumsababishia majeraha. Pamoja na kueleza kuumia vibaya kutokana na
tukio hilo, Happines aliwashukuru wafanyakazi wa Hospitali ya Mkoa wa
Kagera kwa huduma nzuri waliyompatia tangu juzi alipofikishwa
hospitalini hapo.
Majeruhi mwingine, Paulina Spilian aliyelazwa hospitalini hapo akiwa
amejeruhiwa miguu alisema akiwa ndani ya nyumba yake ghafla alisikia
mtikisiko mkubwa ulioambatana na kishindo cha kuanguka kwa kuta za
nyumba na akiwa katika harakati za kutaka kukimbia nje aliangukiwa na
ukuta miguuni.
Majeruhi huyo aliiomba Serikali kuwasaidia kwa kuwajengea nyumba na
pia kuwapa elimu kuhusiana na matukio kama hayo ili waweze kujiokoa
baada ya kuona dalili au viashiria tofauti na ilivyotokea juzi.
Advela Respicius ambaye ni mama wa marehemu, Verdiana Respicius
aliyekufa baada ya kufunikwa na kifusi cha nyumba, akizungumza kwa niaba
ya familia za wafiwa wa tukio hilo, alitoa shukrani kwa serikali kwa
kutoa majeneza, sanda na usafiri wa kuwapeleka marehemu hao mpaka
vijijini kwa ajili ya maziko.
Vifaa vya kutabiri kufungwa Wakati hofu ikiwa bado imetawala kutokana
na tukio hilo hasa kutokana na wananchi wa Kagera kueleza kutofahamu
lolote kabla ya kutokea kwa tetemeko kutokana na kutopewa taarifa zozote
na mamlaka za serikali, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson
Mandela kilichopo eneo la Tengeru, mkoani Arusha kimesema kinatarajia
kuanza kufunga vifaa vitakavyotoa ishara ya matukio ya matetemeko ya
ardhi kabla majanga hayo kutokea.
Katika mradi huo maalumu chini ya Kitengo cha Utafiti wa Miamba na
Volcano, chuo hicho kitashirikiana na taasisi mbalimbali za elimu ya juu
zilizopo Ulaya na Marekani, lakini hasa Chuo Kikuu cha Glasgow
kilichopo Scotland, kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa taasisi hiyo, Profesa
Burton Mwamila.
Katika mradi huo wa kwanza nchini unaolenga kutoa utabiri wa matukio
ya matetemeko na ulipukaji wa volcano nchini, vifaa maalumu
vitakavyokuwa vinapima uwezekano wa kutokea majanga hayo, vitafungwa
katika maeneo nyeti kama milima, vilima na sehemu ambazo huwa na volcano
hai.
Mtaalamu wa miamba ambaye pia ni Mkuu wa Taasisi ya 'Eco Science'
inayoshughulika na utafiti wa miamba pamoja na milipuko ya volcano, Dk
Ben Beeckmans amefafanua kuwa 'Mlima wa Mungu' (Oldonyo Lengai) uliopo
eneo la Ngaresero, wilayani Ngorongoro ndio chanzo kikubwa cha
matetemeko ya ardhi katika eneo lote la Afrika Mashariki. Mlima huo
wenye volkano hai pia umekuwa ukilipuka mara kwa mara na tukio la mwisho
lilirekodiwa mwaka 2007.
Vifaa hivyo vya kutabiri matetemeko ya ardhi vitafungwa kuzunguka
eneo la mlima huo, Ziwa Natron, Mlima Meru na hata Mlima Kilimanjaro
pamoja na maeneo mengine nchini.
Lakini hatua hiyo si kwamba imetokana na matukio ya tetemeko
yaliyoyakumba maeneo mengi ya nchi juzi bali ni mpango uliobuniwa na
wataalamu mapema mwaka huu na kwamba kilichobaki ni utekelezaji tu.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika Taasisi ya Sayansi na
Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Karimu Meshaki alisema atatoa
taarifa rasmi kuhusu maendeleo ya mpango huo wiki hii.
Hivi karibuni Serikali ilijenga maabara kubwa kabisa ya utafiti wa
kisayansi katika Chuo cha Nelson Mandela, Arusha ambayo ilizinduliwa
miezi miwili iliyopita.
Serikali ya India pia ilitoa mchango wake kwa kukipatia chuo hicho
kompyuta kubwa na yenye uwezo mkubwa zaidi nchini ijulikanayo kama
'Param Kilimanjaro,' ambayo pamoja na shughuli nyingine pia inatarajiwa
kutumika katika tafiti za miamba, gesi asilia na pia kwenye huu mradi
mpya wa kufuatilia matukio ya tetemeko la ardhi na milipuko ya volkano.
Post a Comment