Header Ads

Leo ni sikukuu ya Idd el Hajj

LEO ni Sikukuu ya Idd el Hajj ambapo Baraza Kuu la Waislamu nchini (BAKWATA), limewataka waislamu nchini kote kusherehekea sikukuu hiyo kwa amani, huku wakiwakumbuka wenye matatizo, kuwa wepesi wa utoa sadaka na isiwe siku ya kutenda maovu.





Katibu Mkuu wa Bakwata, Shehe Suleiman Lolila alitangaza jana kuwa leo ni Sikukuu ya Idd El Hajj na kuongeza kuwa kitaifa sherehe hizo, zitafanyikia Makao Makuu ya Bakwata yaliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Alisema mgeni rasmi katika sherehe hizo, anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambapo sala itaanza mapema saa moja asubuhi na Baraza la Idd kuanza saa 2:30 hadi saa 4:00 asubuhi.
Idd El Hajj inahitimisha Ibada ya Hijja kwa waumini mbalimbali wa dini ya kiislamu huko Makka nchini Sauda Arabia, ambayo ni miongoni mwa nguzo tano za dini ya kiislamu ambayo hutakiwa kutekelezwa mara moja kwa mtu mwenye uwezo wa kifedha.

Katika hatua nyingine; Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein atakuwa mgeni rasmi katika Baraza la Idd, litakalofanyika katika Shule ya Mkanyageni Wilaya ya Mkoani Pemba huku sala ya Idd ikifanyika katika Msikiti uliopo Bandarini Mkoani. Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Wakfu na Mali ya Amana.
Katika taarifa hiyo, Mufti wa Zanzibar, Shehe Saleh Kabi ataongoza sala ya Idd ambapo Baraza la Idd litahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali wakiwemo mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano.

Katika baraza hilo, Rais Shein anatazamiwa kutoa hotuba ambayo ni mwongozo na dira kwa wananchi ambayo hulenga katika maeneo mbalimbali ikiwemo siasa na mipango ya maendeleo ya nchi, ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman alisema maandalizi yake yalikuwa yamekamilika tangu jana.

Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na wafanyakazi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), ambayo ni wachapishaji wa Magazeti ya Daily News, Sunday News, HabariLeo, HabariLeo Jumapili na SpotiLeo, wanawatakia Watanzania wote sikukuu njema.

No comments