Header Ads

MKUU wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe na wakurugenzi wa mji na wilaya ya Handeni

MKUU wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe na wakurugenzi wa mji na wilaya ya Handeni wamefanikiwa kusuluhisha mgogoro wa mpaka uliodumu kwa muda mrefu kati ya mtaa wa Mankinda, kijiji cha Konje kilichopo Halmashauri ya Mji na Kijiji cha Kweditilibe kilichopo wilayani Handeni.





Akizungumza na wananchi wa vijiji hivyo, Gondwe amesema mwenye mamlaka ya ardhi yote ya Tanzania ni Rais John Magufuli pekee na ndiye anayeweza kubadili matumizi ya ardhi.
Amesema ramani ya mwaka 2007 ndiyo inayotambulisha mipaka ya maeneo husika Tanzania nzima, na kwa maana hiyo hata mgogoro uliopo kati ya kijiji cha Kweditilibe na mtaa wa Mankinda utatatuliwa kwa ramani ya 2007 na tangazo la serikali la mwaka 2011 lililotumika kuitangaza Halmashauri ya Mji wa Handeni.
Amewaeleza wananchi kuwa lengo kuu la kugawanya halmashauri hizo lilikuwa ni kusogeza huduma za kijamii karibu na wananchi, na kwamba mipaka ya maeneo haizuii shughuli nyingine za kimaendeleo kufanyika.
Mkurugenzi wa Mji wa Handeni, Keneth Haule alisema ipo haja ya wananchi kumaliza mgogoro ili waweze kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo. Naye Mkurugenzi wa Wilaya ya Handeni, William Makufwe aliwaeleza wananchi kwamba,
“Hatutengenezi mipaka mipya badala yake tunasimamia ramani iliyokuwepo na tangazo la serikali la mwaka 2011 lililotumika kuitangaza Halmashauri ya Mji wa Handeni. Kikundi ama mtu atakayekwenda kinyume na ramani iliyopo atakuwa ameenda kinyume na ulinzi wa amani, ambapo Mkuu wa Wilaya ambaye ni Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama atamchukulia hatua kwa sababu hakuna mtu yeyote anayekubaliwa kuharibu mipaka ya kiutawala,” amesema.
Wataalamu kutoka Halmashauri ya Mji na Wilaya walisoma ramani na Tangazo la Serikali (GN), ili kupata mpaka unaotenganisha mtaa wa Mankinda uliopo katika kijiji cha Konje Halmashauri ya Mji wa Handeni na kijiji cha Kweditilibe kilichopo Halmashauri ya Handeni Vijijini.
Wananchi wa vijiji vya pande zote mbili waliridhia kwamba kila mmoja anajua mpaka wake. Ramani ya 2007 ndiyo iliyotumika kusuluhisha mgogoro ambo ulikuwepo pia katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni uliohusisha kijiji cha Gendagenda na Kwabojo.

No comments