Header Ads

MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Hassan Abasi amesema, atahakikisha serikali inasema kwanza kabla ya wengine kusema.

MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Hassan Abasi amesema, atahakikisha serikali inasema kwanza kabla ya wengine kusema.






Ameyasema hayo leo mjini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Tovuti ya Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA). Abasi ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari (MAELEZO). Amesema, wameanza kukimbizana kwenye michakato ya kuisemea serikali.
“Serikali inapaswa kujisemea, nitahakikisha tunakuwa na serikali inayosema kabla wengine hawajaisemea,” amesema.
Amesema, dunia ina watu bilioni saba na kati yao, bilioni tatu wanatumia mitandao ya kijamii hali inayomaanisha nusu ya dunia iko kwenye mitandao. Alisema, duniani kuna mitandao zaidi ya 200 na kila mtandao ni maarufu.
“Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 91 ya kampuni kubwa kama Sony na Phillips zina mitandao miwili hadi mitano ya kijamii na wengi duniani wanaondoka kwenye mfumo wa kutegemea magazeti na televisheni,” amesema.
Amesema Serikali kwa upande wake, inatumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kusambaza habari.
“Tunavyoongea kuna timu ya maofisa habari wa serikali wanafanya kazi ya kutumia habari, picha hata video kwenye mitandao,” amesema.
Amesema wananchi wengi wanatumia mitandao ya kijamii kwa kuwa ni bure ukiwa na bando tu, unafahamu kitu gani kinaendelea duniani.
“Mwanzoni watu wa serikali walikuwa waoga kutumia mitandao ya kijamii, sasa wanaitumia, kwani faida yake ni kubwa na dunia haiwezi kuacha aina hiyo ya mawasiliano,” amesema.
Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha, amesema tovuti hiyo ina lengo la kurahisisha utendaji kazi wa serikali na utoaji wa habari kwa umma na tayari imeandaliwa rasimu ambayo itatoa dira na uelekeo mpana kwa lengo kuimarisha na kuboresha utendaji wa kazi na utoaji wa huduma.
Amesema, serikali imedhamiria kuwa na mfumo madhubuti na miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), kwani ni miongoni mwa masuala muhimu kwani mitandao huwezesha wananchi kupata huduma. Naibu Waziri huyo alisema, tovuti hiyo itakuwa na masuala muhimu na kutaka iwe zaidi ya maktaba, kwani tovuti nyingi za serikali zinazoanzishwa zimekuwa si endelevu.
“Tovuti ni maktaba iliyo hai ni lazima iendelee kuboreshwa tovuti nyingine hazibadilishwi, taarifa zinakuwa zile zile tangu tovuti ilipotengenezwa,” amesema.
Ametaka tovuti hiyo iendelee kuwa hai ili watu wengi wapate taarifa mpya kila wakati.
“Ukianzisha tovuti na watu hawaitembelei ujue ina kasoro, tusizindue na tukaondoka, uzoefu unaonesha tovuti nyingi za wizara ni kama zimekufa maofisa habari wake wana changamoto nyingi na ukiwauliza wanakuambia ni ukosefu wa fedha.”

No comments