KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro,atoa tamko
KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, ametoa
rai kwa wakazi wa jiji hilo na wageni wanaoingia jijini humo kutoka
katika mikoa mbalimbali kupuuza taarifa za sauti zinazosambazwa kwenye
mitandao ya jamii kuwa polisi wanawakamata hovyo wanaolala mchana kwenye
nyumba za wageni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Sirro leo,
habari zinazosambazwa
katika mitandao ya WhatsApp naTelegram, pamoja na zilizochapishwa
kwenye baadhi ya magazeti kuwa polisi wanawakamata watu hao kwa madai ya
uzururaji na uzembe ni uvumi.
Kamanda Sirro alisema kwa nia ovu, taarifa hizo zimedai kuwa hatua
hiyo ni kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la 'Hapa Kazi Tu', jambo
ambalo si la kweli.
“Ninawatoa hofu raia wema kuwa tunaendeleza operesheni kuwasaka
watuhumiwa wa makosa mbalimbali wakiwemo wanaofanya biashara ya nyumba
za kulala wageni kinyume cha sheria kwa kuendesha gesti bubu," amesema.
Amesema katika taarifa yake hiyo kuwa uchunguzi umebaini kuwepo na
nyumba za kulala wageni zinazoendesha biashara kiholela kwa kuhifadhi
wahalifu, wakiwemo wanawake na wanaume wanaouza miili yao (dada na kaka
poa).
“Ni wajibu wa polisi kufanya ukaguzi mara kwa mara kwenye nyumba za
wageni, hoteli, migahawa, vilabu vya vileo na kumbi za starehe
zinazokesha," alisema na kuongeza kuwa watakaobainika watachukuliwa
hatua za kisheria.
Sirro amewataka wafanyabiashara wa nyumba za kulala wageni kufuata
taratibu za kupokea wageni kwa kuandika majina yao kwenye vitabu,
kuandika namba za vitambulisho vyao na sehemu wanazotoka na
watakapomtilia mashaka mteja yeyote watoe taarifa kwenye kituo chochote
cha Polisi.
Aliwataka wenyeviti wa Serikali za Mitaa na wajumbe wa Nyumba 10
wawajibike kuwatambua wageni wote wanaoingia kwenye himaya zao na
kuwachukulia hatua stahiki wanaobainika kuwa ni wahalifu, ili kuimarisha
usalama.
Post a Comment