tunapokea wastani wa majeruhi kati ya 50 na 60 kwa siku,
WASTANI wa Sh milioni mbili zinatumika kumtibu majeruhi mmoja wa
pikipiki, jambo ambalo limezifanya hospitali zinazowapokea majeruhi hao,
kuzidiwa na gharama hizo za matibabu.
Madaktari kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) wamesema kwamba
kwa sasa kila siku, wanapokea wastani wa majeruhi kati ya 50 na 60,
jambo ambalo linaiwia vigumu taasisi hiyo kutoa huduma za uhakika kwa
majeruhi hao.
Gharama hizo zinatokana na vyuma vinavyotumika kuwatibu majeruhi wa
mifupa mirefu kuagizwa nje ya nchi, jambo ambalo linaelezwa na madaktari
kwamba kutokana na idadi ya majeruhi kuongezeka kila siku, inailazimu
MOI kukabiliwa na upungufu wa vifaa hivyo.
Kutokana na kuongezeka kwa majeruhi hao wa bodaboda, Jumuiya ya
Madaktari Wakristo (TCMA) wametumia mkutano wao wa mwaka uliomalizika
juzi, kujadili jambo hilo na kueleza kuwa ajali zinazotokana na bodaboda
ni janga la taifa kutokana na kuziongezea gharama za upasuaji
hospitali.
Kwa hali hiyo, wameziomba mamlaka za masuala ya usalama barabarani,
kuhakikisha zinatunga sheria kali zitakazowabana wapanda na waendesha
bodaboda ili kuepusha taifa kuwa na
walemavu wengi wa ajali za vyombo
hivyo vya usafiri.
Madaktari kutoka MOI katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini
Dar es Salaam, walisema taasisi hiyo kwa sasa imelemewa na majeruhi wa
bodaboda, jambo ambalo linafanya vifaa na miundombinu ya taasisi hiyo,
kutotosheleza mahitaji na hivyo kufanya gharama zinazotolewa kwa
majeruhi hao kuwa hafifu.
Madaktari hao katika mkutano wao wa mwaka wa 79 ambao ulimalizika
juzi kwenye ukumbi wa AMECEA, Dar es Salaam, waliwaita wadau mbalimbali
wakiwemo madereva wa bodaboda, Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini
(Sumatra), polisi wa Usalama Barabarani, madaktari, maofisa wa Shirika
la Afya Duniani (WHO) na waandishi wa habari, kujadili namna gani taifa
linaweza kupunguza ajali za bodaboda.
Rais wa TCMA, Dk Isaya Tosiri alisema wamelazimika kutumia mkutano
huo kujadili ajali zinazotokana na bodaboda kwa sababu hospitali ambako
wanafanya kazi madaktari hao Wakristo zimelemewa kutokana na kupokea
majeruhi wengi wa pikipiki.
"Kwa kweli hospitali zetu za makanisa zinapokea sana majeruhi wengi
wa bodaboda, kila daktari aliyeko hapa analalamika kuongezeka kwa
majeruhi huku hospitali zetu hazina uwezo wa kuhimili ongezeko hili,
ndio maana tunasema ni janga la taifa ni lazima wadau watafute
suluhisho," alisema Dk Tosiri.
Daktari Bingwa wa Hospitali ya Rufaa ya Nkinga, Yohana Masota iliyoko
mkoani Tabora alisema katika hospitali yake wanapokea wastani wa
majeruhi 10 kila siku ambao wanatokana na ajali za pikipiki jambo ambalo
linafanya hospitali hiyo kuwa na mzigo wa kutibu majeruhi.
"Naamini kwamba ajali nyingi zinatokana na madereva hawa kutokuwa na
uelewa wa sheria za barabarani ndio maana wanapata ajali mara kwa mara,
ni lazima hatua zichukuliwe maana hospitali zetu zinalemewa," alisema Dk
Masota.
Daktari Bingwa wa MOI, Victoria Munthali amesema zamani kabla ya
kuruhusiwa kwa bodaboda kubeba abiria wa biashara, taasisi yake ilikuwa
inapokea majeruhi wasiozidi watano kwa siku na siku ambako kuna ajali ya
basi waliweza kupokea wastani wa majeruhi 10 kwa siku.
"Lakini siku hizi tunapokea wastani wa majeruhi kati ya 50 na 60 kwa
siku, miundombinu ni ile ile hivyo uwezo wetu wa kuwahudumia unakuwa
mdogo," amesema Dk Munthali.
Ameongeza kuwa hata vifaa kama vyuma, ambavyo ndivyo vinavyotumika
kuwatibu majeruhi wa mifupa mirefu, kifaa cha gharama za chini kinauzwa
dola za Marekani 70 (takribani Sh 147,000)
"Kwa wale ambao wanavunjika mgongo 'screw' zinazotumika kuwatibu ya
gharama za chini ni dola za Marekani 200 (sawa na Sh 420,000).
Dk Boniface Respicious ambaye ni daktari bingwa wa mifupa wa MOI,
alisema gharama za kumtibu majeruhi mmoja wa ajali ya bodaboda ni Sh
milioni 2 jambo ambalo limefanya hospitali nyingi kulemewa na mzigo wa
majeruhi.
Amependekeza kuanzishwe mfuko maalumu wa majeruhi kama ilivyo kwa
mifuko mingine ya umeme vijijini (Rea) ambao utasaidia kutibiwa kwa
majeruhi wa ajali za bodaboda na magari.
Alisema fedha za mfuko huo zikatwe wakati mmiliki wa gari au bodaboda
anapoenda kukata leseni ya matumizi ya barabarani kama inavyofanyika
sasa kwa Zimamoto.
"Hizi kampuni za bima hazisaidii lolote kwenye matibabu wakati
wanachukua fedha nyingi, nadhani ukianzishwa mfuko wa majeruhi
utaisaidia serikali kuwa na fedha za kutosha za kutibu majeruhi na
itasaidia kupunguza mzigo ulioko kwenye hospitali zetu," alisema Dk
Respicious.
Alisema kwa sasa huduma za kuwatibu majeruhi zimedorora katika
hospitali nyingi kutokana na kukosa fedha za kununulia vifaa pamoja na
dawa kutokana na ongezeko la majeruhi wa bodaboda.
Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii, Dk
Josphine Ballati alisema vifo vinavyotokana na ajali za bodaboda ni
nyingi kuzidi vifo vinavyosababishwa na baadhi ya magonjwa.
"Huu ni ugonjwa mwingine ambao taifa letu limepata, lazima tutafute suluhisho."
Alionya kuwa kama taifa halitachukua hatua, miaka 20 ijayo nguvu kazi
nyingi za taifa watakuwa ni walemavu kutokana na usafiri wa bodaboda
kutumiwa na watu wengi. Alisema pia hatua zichukuliwe, kuhakikisha
zinalipunguzia gharama taifa kuwatibu majeruhi hao.
Mkurugenzi wa Barabara wa Sumatra, Johansen Kahatano alisema imekuwa
ngumu kuwadhibiti madereva wa bodaboda kwa sababu vijana wengi
wanaofanya biashara hiyo ni wale ambao walikuwa na tabia za ajabu huko
nyuma.
"Hawa ni vigumu kujifunza na kama wakijifunza ni ngumu kuelewa,"
alisema Kahatano na kusisitiza kuwa serikali inafanya jitihada kufanya
usafiri huo baadaye uwe na heshima na kupunguza matatizo ya sasa.
Post a Comment