Header Ads

MKUU wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe akishirikiana na kamati yake ya Ulinzi na Usalama wamefanikiwa kukamata kete 88 za dawa





MKUU wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe akishirikiana na kamati yake ya Ulinzi na Usalama wamefanikiwa kukamata kete 88 za dawa za kulevya aina ya mirungi zilizokuwa zimefungwa kwa mtindo wa vifurushi kwa kutumia kamba za migomba.
Tukio hilo la kukamata dawa hizo limetokea katika kijiji cha Mzeri, kata ya Misima ambapo Gondwe alibainisha kuwa wilaya hiyo ina matumizi makubwa ya mirungi na bangi.
Imeelezwa kuwa dawa hizo zilikua zikisafirishwa kutoka Korogwe na kwamba mtuhumiwa alifanikiwa kuwatoroka polisi na jitihada za kumtafuta ili kumfikisha kwenye vyombo vya sheria zinaendelea.
“Vijana wetu wa upelelezi wamegundua utumiaji wa dawa hizo na tutahakikisha tunawafikisha kwenye vyombo vya sheria wauzaji na watumiaji wa dawa hizo,” alisema.
Aliongeza kuwa polisi inashirikiana na zimamoto na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kudhibiti kabisa biashara hiyo.
“Tumeunda timu ambayo mwenyekiti wake ni OCD itakayokuwa inafanya doria usiku na mchana ili kuhakikisha vijana wetu wanabaki salama na kukomesha kabisa biashara ya dawa za kulevya,” alisema.
Mkuu huyo wa wilaya alitoa wito kwa watumiaji na wauzaji wa dawa hizo kuacha mara moja badala yake wajikite kwenye shughuli nyingine halali zitakazoweza kuwainua kiuchumi.
“Jeshi la polisi halitaacha kuwafuatilia na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kwani Serikali wilayani Handeni haitakuwa tayari kuona nguvu kazi ya vijana inateketea,” alisema.
Baadhi ya vijana wilayani humo wameunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kupambana na dawa za kulevya na wamesema kuwa nguvu kazi ya vijana wengi imekuwa ikiteketea kutokana na utumiaji wa dawa hizo

No comments