YANGA YAICHEZESHA STAND KINDUBWE NDUBWE 4-0
MABINGWA watetezi wameanza kwenda kasi kuelekea lilipo taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia kuitandika mabao 4-0 Stand United jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, kikosi cha kocha Mzambia, George Lwandamina kinafikisha pointi 48 baada ya kucheza mechi 21, kikiendelea kuongoza Ligi Kuu, kikifuatiwa na vijana wa Mcameroon, Joseph Marius Omog, Simba SC wenye pointi 44 za mechi 20.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Suleiman Kiungani wa Morogoro, aliyesaidiwa na Mohammed Mkono wa Tanga na Abdallaah Shaka wa Taborea, hadi mapumziko Yanga ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-0 kupumzika ikiwa inaongoza mabao 2-0.
Mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Dombo Ngoma aliyekuwa anacheza kwa mara ya kwanza baada ya wiki nne, aliipatia Yanga bao la kwanza dakika ya 17 kwa kichwa akimalizia krosi nzuri ya winga Simon Happygod Msuva.
Msuva akaifungia Yanga SC bao la pili dakika ya 26 akimalizia krosi ya Haruna Niyonzima, hilo likiwa bao lake la 10 msimu huu na sasa anaongoza kwa mabao Ligi Kuu, akimuavha winga wa Simba, Shiza Kichuya anayebaki na mabao yake tisa.
Baada tu ya kuanza kwa kipindi cha pili, kiungo mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa akaifungia Yanga bao la tatu dakika ya 46 kwa shuti la mbali baada ya pasi ya Thabani Kamusoko.
Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alamalizia kona ya beki wa kulia, Juma Abdul kuipatia Yanga bao la nne kwa kichwa dakika ya 68.
Baada ya bao hilo, Stand United wakabadilisha kipa, wakimtoa Sebastian Stanley na kumuingiza Mohammed Makaka ambaye alijitahidi kwenda kudaka bila kuruhusu bao.
Kikosi cha Yanga kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Mngwali, Kevin Yondan/Andrew Vincent ‘Dante’, Justin Zulu, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma/Juma Mahadhi, Obrey Chirwa na Haruna Niyonzima/Emmanuel Martin.
Stand United; Sebastain Stanley/Mohammed Makaka, Jacob Massawe, Erick Mulilo, Adeyum Ahmed, Revocatus Richard, Ibrahim Job, Abdulaziz Makame, Adam Salamba, Frank Khamis/Amri Kiemba, Abasalim Chidiebele/Aaron Lulambo na Suleiman Kassim ‘Selembe’.
Post a Comment