WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema inawezekana kuwasajili watoto wote nchini
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema inawezekana kuwasajili watoto wote nchini na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa.
Mwakyembe aliyasema hayo katika hafla ya kukabidhi tuzo zilizotolewa na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa viongozi wa mikoa ya Iringa na Njombe.
Ilikuwa ni hatua ya kuwapongeza na kutambua mchango wao katika kufanikisha utekelezaji wa mpango wa kuwasajili na kuwapa vyeti vya kuzaliwa watoto wa umri chini ya miaka mitano katika mikoa yao.
“Iringa na Njombe wameweza kusajili watoto kwa asilimia 100 kwa kipindi cha miezi minne, hivyo kama mikoa mingine itaiga mfano kwa mikoa hii basi serikali itaweza kukamilisha, ndani ya muda mfupi, kuwasajili na kuwapa vyeti vya kuzaliwa watoto wote walio na umri chini ya miaka mitano,” alisema.
Alieleza kwamba mikoa ya Mwanza, Mbeya na Songwe imekuwa ikitekeleza mpango huu kwa zaidi miaka mitatu lakini mpaka sasa hawajafikia kusajili watoto kwa asilimia 80, hivyo akakasisitiza viongozi wahakikishe suala hilo linafanikiwa.
Kwa mujibu wa maelezo ya awali yaliyotolewa na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Emmy Hudson, hali ya usajili katika mikoa ya Iringa na Njombe ilikuwa sio ya kuridhisha kwani ni watoto asilimia 11.7 katika mkoa wa Iringa na asilimia 8.5 katika mkoa wa Njombe ndio walikuwa wamesajiliwa.
“Hivi karibuni tutaanza utekelezaji wa mpango huu katika mikoa ya Shinyanga na Geita na tutatumia uzoefu tulioupata katika mikoa ya Iringa na Njombe ili kuhakikisha na huko tunapata mafanikio makubwa kwa kipindi kifupi” alissema Hudson.
Katika hafla hiyo Mwakyembe alikabidhi tuzo na hati za pongezi kwa halmashauri 11, Ofisi zote za wakuu wa wilaya za mikoa ya Njombe na Iringa na kwa ofisi za za wakuu wa mikoa hiyo.
Post a Comment