Header Ads

SERIKALI imeuondoa bungeni Muswada wa Sheria ya Madaktari,


Naibu Spika, Dk Tulia Ackson

SERIKALI imeuondoa bungeni Muswada wa Sheria ya Madaktari, Madaktari wa Meno na Wataalamu wa Afya Shirikishi wa Mwaka 2016.
Akitangaza agizo hilo bungeni Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alisema serikali imeamua kuuondoa muswada huo kwa sasa.
“Hilo ni agizo la serikali,” alisema Dk Tulia wakati akiahirisha Bunge jana asubuhi.
Akizungumza na gazeti hili, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla alisema serikali imeuondoa muswada huo kutokana na wadau wa sekta ya afya kutoridhika kwamba hawajatendewa haki.
Alisema japo wadau hao, waganga wasaidizi na waganga wasaidizi wa meno, walishirikishwa katika kutoa maoni kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, inaonekana hawajaridhika kutokana na kitendo cha kutoingizwa rasmi kwenye jina la muswada huo, kitendo ambacho wanaona ni kama dalili za kuondolewa kazini kama ungepitishwa.
Alisema hakuna anayekataa kwamba hao ni wataalamu muhimu katika sekta ya afya, isipokuwa hawawezi kutambuliwa kama madaktari kutokana na ukweli kwamba mtu anatambuliwa kuwa daktari kama ana shahada ya kwanza, sio chini ya hapo.
Aliongeza kuwa, kumekuwa na tafsiri kwamba wataondolewa kazini au watazuiwa kutoa huduma ya afya, ukweli ni kwamba kutoandikwa kwenye jina la muswada, hakumaanishwi kwamba waaondolewa kazini, wataendelea na kutoa huduma kama watoa huduma wengine wenye cheti, diploma, shahada ya kwanza, uzamili na uzamivu.
“Kada hiyo haifutwi, kwani ni kada yenye watoa huduma wengi zaidi ya 13,000 ni muhimu katika kutoa huduma hasa ya upasuaji kinamana wakati wa kujifungua na wanaizidi idadi ya madaktari ambao ni takribani 3,000, na wao ni waajiriwa wa serikali,” alisema.
Alisema kitaaluma, daktari na daktari msaidizi ni watu wawili tofauti, kwani mtu akitaka kusoma udaktari lazima asome miaka mitano zaidi ya ile elimu ya elimu ya stashahada anayosoma daktari msaidizi, hivyo si halali wakaitwa madaktari.
Akitoa maoni yake, Mjumbe wa Kamati ya Kamati ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jajii, Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile (CCM) alisema kuletwa kwa muswada huo kujadiliwa bungeni ulikuwa unafuta ule wa mwaka 1959 na hivyo ungeleta kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya afya.
Muswada huo ungepitishwa ulikuwa unapanua wigo wa usajili wanataaluma, taaluma yenyewe na maadili ya kazi kwa ajili ya watoa huduma mbalimbali katika sekta hiyo wakiwamo madaktari, waganga na matibabu na watoa huduma ya afya shirikishi.

No comments