Header Ads

Watanzania 515 wako gerezani kwa dawa za kulevya

Serikali imesema takwimu za jumla zinaonesha kuwa hadi sasa Watanzania 515 wamekamatwa na kufungwa gerezani kwa makosa ya kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya katika nchi mbalimbali duniani.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Takwimu hiyo imetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo jioni bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa sita wa Bunge la 11, ambapo pamoja na mambo mengine amezungumzia idadi ya watu ambao hadi sasa wamekwishakamatwa katika nchi mbalimbali.
“Nchini China Watanzania walioko magerezani ni zaidi ya 200; Brazili kuna Watanzania 12; Iran wako Watanzania 63; Ethiopia Watanzania saba na Afrika Kusini wako Watanzania 296,” amesema.
Amesema serikali itapambana na janga la dawa za kulevya na kwa dhati bila kumuonea mtu yeyote na kwa kuzingatia misingi ya sheria na haki.
“Lengo la Serikali ni kuwasaidia walioathirika na dawa za kulevya na kuwachukulia hatua kali wale waliowaathiri kwa maana ya wauzaji na wasambazaji. Dhamira ya Serikali ni kupambana na janga hili kwa dhahiri na kwa dhati bila kumuonea mtu yeyote na kwa kuzingatia misingi ya sheria na haki,” amesema.
Waziri Mkuu amesema moja ya hoja za Kamati za Kudumu za Bunge iliyojadiliwa na kuibua hisia kali katika mkutano huu wa Bunge ni kuhusu vita inayoendelea nchini dhidi ya dawa za kulevya na akawaomba Watanzania wote waiunge mkono Serikali juu ya vita hiyo.
“Dawa za kulevya ni hatari sana kwa usalama na ustawi wa Taifa letu. Vita hii inayopiganwa sasa dhidi ya uagizaji, uzalishaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa. Sote tunapaswa kuunga mkono jitihada hizo,” amesisitiza.
Amesema dawa hizo za kulevya, huingia zaidi kutumia njia za bandari bubu kupitia Bahari ya Hindi na mipakani kwa njia ya magari binafsi au mabasi kupitia nchi za Kenya, Uganda na Mpaka wa Tunduma.

No comments