Alisema uhusiano kati ya Tanzania na India umesaidia kunufaisha wananchi wa nchi hizo mbili hasa katika masuala ya kibiashara, miradi ya maendeleo na hivyo kusisitiza ni vyema uhusiano huo ukaendelezwa na kudumishwa.
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema serikali itaendelea kudumisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na India uliodumu kwa muda mrefu hasa katika sekta mbalimbali zikiwemo za elimu, afya na biashara.
Aliyasema hayo jana alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa India nchini, Sandeep Arya, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Alisema uhusiano kati ya Tanzania na India umesaidia kunufaisha wananchi wa nchi hizo mbili hasa katika masuala ya kibiashara, miradi ya maendeleo na hivyo kusisitiza ni vyema uhusiano huo ukaendelezwa na kudumishwa.
Aidha, kupitia kwa Balozi Arya pia ameiomba Serikali ya India kuisaidia Tanzania katika mpango utakaosaidia wakulima kupata taarifa mbalimbali zinazohusu kilimo na masoko ya bidhaa zao kupitia simu za mkononi ili kuondoa usumbufu mkubwa wanaoupata kwa sasa, hasa kuhusu masoko.
Balozi Arya amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa India itakuwa bega kwa bega na Tanzania katika kuhakikisha wananchi wa pande zote mbili wananufaika na uhusiano uliopo.
Aidha, alisema India itaendelea kuisaidia Tanzania katika uimarishaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na miradi ya maendeleo na uimarishaji wa shughuli za kiuchumi.
Wakati huo huo, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan jana alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Sudan nchini, Mahgoub Sharfi, mazungumzo yaliyolenga pamoja na mambo mengine, kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Sudan.
CHANZO HABARI LEO
Post a Comment