Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imechukua usimamizi wa benki ya Twiga Bancorp Ltd kutokana na upungufu mkubwa wa mtaji
Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imechukua usimamizi wa benki ya Twiga Bancorp Ltd kutokana na upungufu mkubwa wa mtaji kinyume na matakwa ya sheria ya mabenki, ambapo hivi sasa benki hiyo inajiendesha kwa hasara ya Sh bilioni 21.
Kutokana na hatua hiyo, BoT imevunja Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya benki hiyo na kwamba ndani ya wiki moja watasitisha huduma kwa lengo la kujipanga jinsi ya kuendesha benki hiyo.
Akitangaza uamuzi huo jana jioni kwa waandishi wa habari Dar es Salaam, Gavana wa BoT, Profesa Beno Ndullu alisema sababu ya uamuzi huo inatokana na benki hiyo kuendeshwa kinyume cha sheria inayopaswa kufuatwa na benki zote, kuna upungufu mkubwa wa mtaji ambao unahatarisha usalama wa sekta ya fedha.
“Tunajua benki hii inamilikiwa na serikali kwa asilimia 100, tulizungumza nao kwa muda sasa inaonekana mtaji wa kuiongezea benki hii hautatolewa tena, kwa hiyo mamlaka inampa gavana kutoa kipindi cha benki kama hiyo kutafuta mtaji na sasa ni wazi kuwa haiwezi kupata mtaji huu tena, tumeamua kuiweka chini ya usimamizi wetu kujaribu kutafuta suluhu ya kuendesha benki hiyo,” alisema Gavana Ndullu.
Alisema uamuzi wa BoT umekuja ili kulinda wateja wa benki hiyo waliowekeza fedha zao pamoja na kulinda usalama wa benki nyingine kwa sababu inapotokea hali kama hiyo kwenye benki moja, kama hatua hazitachukuliwa inaweza kusababisha benki nyingine kuanguka.
Kuhusu wafanyakazi, Gavana Ndullu alisema wataendelea kuwepo kwa sababu kinachobadilika ni Msimamizi wa Benki ambaye atashughulika na watumishi na kuwatoa hofu kuwa wao si sehemu ya menejimenti hivyo wataendelea kuwepo.
Hata hivyo, Gavana Ndullu aliwaonya wale wote wanaodaiwa na benki hiyo kuhakikisha wanarejesha fedha walizokopa, kwa sababu sheria ina mkono mrefu na watasakwa popote ili kulipa fedha walizokopo na ikibidi mali zao kushikiliwa ambazo waliweka dhamana.
Post a Comment