Header Ads

Baraza la Taifa la Usalama Barabarani lina mkakati wa kupunguza ajali ndani ya miezi sita umetajwa kuvuka malengo yaliyowekwa katika kipindi cha miezi miwili pekee.

 Baraza la Taifa la Usalama Barabarani  lina mkakati wa kupunguza ajali ndani ya miezi sita umetajwa kuvuka malengo yaliyowekwa katika kipindi cha miezi miwili pekee.




Mkakati huo uliozinduliwa Agosti, mwaka huu una lengo la kupunguza ajali za barabarani kwa asilimia 10, umevuka lengo katika kipindi cha miezi miwili na kufikia asilimia 18.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, alisema hayo jana alipotoa tathmini ya utekelezaji wa mkakati huo katika kipindi cha miezi miwili.
Masauni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, alisema tathmini hiyo inaonesha kabla ya kuanza kwa mkakati huo kulitokea ajali 577 na miezi miwili baada ya kuanza kwake zilitokea ajali 471, ambazo zinaonesha kuna upungufu wa ajali 106 ambazo ni sawa asilimia 18.
“Kwa kipindi hicho cha miezi miwili kabla ya mkakati kulitokea vifo 467 na baada ya mkakati kulitokea vifo 367. Hii inaonesha kuwepo kwa upungufu wa vifo 91 ambavyo ni sawa na asilimia 19,” alisema Masauni.
Aliongeza kuwa katika miezi hiyo miwili kabla ya mkakati kulitokea majeruhi 810 na baada ya mkakati huo kulitokea majeruhi 496 ambao ni upungufu wa majeruhi 314 sawa na asilimia 39.
Akizungumzia kuhusu ajali za pikipiki, alisema kabla ya mkakati huo kulitokea ajali za pikipiki 200 na baada ya mkakati zilipungua hadi 170 ambazo ni sawa na asilimia 15.
Pia vifo 124 vilitokea lakini baada ya mkakati huo kulitokea vifo 118 na kuonesha upungufu wa vifo sita ambavyo ni sawa na asilimia tano. Kabla ya mkakati huo kulitokea majeruhi 135 lakini miezi miwili baada ya utekelezaji wa mkakati huo walipungua hadi kufikia 113 na kuonesha upungufu wa majeruhi 22 ambao ni sawa na asilimia 16.
Katika hatua nyingine, Masauni alisema, kabla ya miezi miwili makosa ya barabarani yaliyokamatwa yalikuwa ni 324,284 lakini baada ya miezi miwili ya mkakati huo makosa yaliongezeka hadi 393,728.

No comments