WASANII wa muziki wa kizazi kipya na wengine wametakiwa kuwakatia risiti wateja wao kwa kutumia mashine za kielektroniki, EFD. Wanatakiwa kutoa risiti hizo baada ya kupokea fedha zao kutoka kwa promota kwa ajili ya kuimba au kufanya kazi yoyote ya sanaa inayohitaji malipo.
Hayo yalisemwa na Meneja wa Elimu na Huduma kwa Mlipa Kodi, Gabriel Mwangosi wakati akizungumza na gazeti hili kuhusu mashine hizo kwa wasanii.
Alisema kuwa wasanii kama watu wengine wafanyao biashara wanatakiwa kuwa ma mashine hizo na kutumia kuwapatia risiti wanaowakodisha kuimba.
Alisema kuwa hiyo itasaidia kuonesha ni kwa kiasi gani wanachangia pato la taifa kwa kulipa kodi itakayokuwa ikioneshwa kwenye mashine hiyo. Alisema kuwa wasanii wanafanya biashara ambapo serikali inatakiwa kunufaika na mapato yatokanayo na kazi hiyo ya sanaa.
"Wasanii ni wafanyabiashara na kila wanachopata kwa njia ya kazi ya sanaa inatakiwa nao kushiriki katika kulipa kodi, ikiwa ni kama mchango wao kwa taifa,"alisema Mwangosi. Serikali imekuwa na shauku ya kuwasaidia wasanii kupata haki zao mbalimbali ambazo zinaonekana kuwa zimekuwa zikidhulumiwa.
Serikali iliyopita ya awamu ya nne ya Jakaya Kikwete ilianzisha utaratibu wa kukata stempu kwa kila kazi ya sanaa na kubandikwa kwenye nakala kuonesha kuwa malipo ya kodi yamefanyika.
Licha ya juhudi hizo lakini bado kumekuwa na wajanja wachache ambao wamekuwa wakiikosesha serikali hiyo hiyo mapato kwa kuchakachua matumizi ya stempu hizo.
Kwa sasa serikali inaendelea na mchakato wa kuwasaidia wasanii kunufaika na kazi zao za sanaa kwa kuwawekea mfumo utakaopelekea wamiliki wa vituo vya habari hasa Radio na Luninga kulipia nyimbo za wasanii watakazokuwa wakizitumia kwenye vyombo vyao.
chanzo habari leo
Post a Comment