Header Ads

Wamachinga kusajiliwa na vitambulisho kupatiwa


Wito umetolewa kwa wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi hususani wamachinga kujisajili na hatimaye kupatiwa vitambulisho maalum kwa lengo la kusaidia biashara zao kutambulika, kukopesheka na kurahisisha mawasiliano ya usimamizi wa biashara hizo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa usajili na utoaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo uliofanyika leo mkoani Arusha, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Fabian Daqqaro amesema ni muhimu wafanyabiashara kutumia fursa hii ya kujisajili ili kurasimisha biashara zao.
"Ni matumaini yangu kuwa, wafanyabiashara wengi wadogo wadogo mkoani hapa, mtatumia fursa hii kujisajili kwa sababu ninafahamu wengi  wenu malengo yenu siyo kuwa wafanyabiashara wadogo muda wote, bali mtakuza biashara zenu na kuwa wafanyabiashara wakubwa na hii itawezesha kuchangia mapato ya Serikali," 
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Kodi za Ndani kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Abdul Zuberi ameeleza kuwa, zoezi hili la kuwasajili na kuwapatia vitambulisho wafanyabiashara wadogo limetokana na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
"Ni ukweli usiopingika kwamba, Rais wetu kwa nyakati tofauti amekuwa akiwapigania na kutaka wafanyabiashara wadogo wadogo kutambulika rasmi na kupatiwa vitambulisho ikiwa ni pamoja na kutafutiwa maeneo rafiki ya kufanyia biashara zao," amesema Zuberi.
Ameongeza kuwa, kutokana na juhudi hizo za Rais Magufuli, Serikali kupitia Kikao cha Bunge la Bajeti la Mwaka wa Fedha 2017/2018, ilifanya marekebisho mbalimbali ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015 ambapo moja ya marekebisho hayo ni kuwatambua na kuwapatia vitambulisho maalum wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi na jukumu hili limekasimiwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania.

No comments