Header Ads

AMLAKA ya Kuendeleza Biashara Tanzania (TanTrade) imesema serikali inatafuta wawekezaji, watakaongeza thamani ya dagaa




AMLAKA ya Kuendeleza Biashara Tanzania (TanTrade) imesema serikali inatafuta wawekezaji, watakaongeza thamani ya dagaa wa Zanzibar, wapate soko zaidi kwenye maduka makubwa nje ya nchi.
Kwa mujibu wa TanTrade, umefanyika utafiti na kubaini pia kuwa chumvi ya Pemba ina soko kubwa hivyo vianzishwe viwanda vya kuisindika kuiongezea thamani iuzwe kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Edwin Rutageruka amesema, mtazamo wa mamlaka hiyo hivi sasa ni kuipeleka chumvi ya Pemba kwenye soko la kimataifa. Rutageruka pia amesema, wafanyabiashara kutoka Ulaya wamebaini fursa iliyopo katika viungo vinavyopatikana Zanzibar ikiwemo hiliki, karafuu na mdalasini.
“Na sasa hivi tumewaunganisha na wafanyabiashara waliopo hapa wa spices (viungo) kwa ajili ya kupeleka kwenye masoko ya Ulaya, na tumewashapeleka vilevile kwenye masoko ya Mashariki ya Kati kwenye maonesho makubwa ya dunia yanayoitwa Gulf Food tuliwapeleka wafanyabiashara wa Zanzibar kama wanne hivi na kwa kweli wanafanya vizuri sana katika kuuza nje viungo,” amesema.
Rutageruka pia amesema, kama kilimo cha mbogamboga na matunda kikiunganishwa na utalii ni fursa kubwa kwa uchumi wa Zanzibar.
“Hapa kuna maembe ya kila aina kwa taarifa yenu, na hotelini nadhani mmegundua tukienda kwenye mahoteli tunapoishi sisi tunakula asubuhi breakfast wanakula matunda yote yanayozalishwa hapa, sasa ukisikia wanasema watalii wastani mwaka 2017 wastani kama 450,000 ukichukua wastani kila mtalii mmoja ale embe moja kila asubuhi kwa embe la shilingi 1,000 unaongelea uchumi wa milioni 450 mathalani…” amesema.
“Unaweza ukaona ni kwa jinsi gani tunda moja tu embe kama likiweza kuwa linked (likiunganishwa) na sekta ya utalii, unaweza kujikuta unatengeneza uchumi mkubwa sana yaani huo ni mfano mmojawapo, hapa kuna mapapai yanazalishwa, kuna ndizi zinazalishwa sasa tuangalie namna gani tunaweza tukalink na sekta ya utalii na sekta ya kilimo tuweze kuzalisha bidhaa zinazokubalika” amesema mjini Unguja alipozungumza na Habarileo wakati wa Jukwaa la Fursa za Biashara Zanzibar.
Amesema, hivi sasa dagaa wa Zanzibar, wanauzwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na bado kuna fursa ya kuwaongezea thamani.
“Hii ni fursa kwa TSN (Kampuni ya Magazeti ya Serikali inayochapisha gazeti hili na magazeti dada ya HabariLEO kila siku, Daily News, SundayNews na SpotiLeo) kuwezesha sisi kukutana na wawekezaji, lakini tuangalie namna gani tunaweza kuwa-link wafanyabiashara na wawekezaji lakini angle yetu sisi tunayoitaka ni kuilink sekta ya utalii na kilimo kusudi tuitoe hii nchi kiuchumi kwa kuzitumia fursa zote zilizopo” amesema hivi karibuni kwenye ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi mjini Unguja wakati wa jukwaa hilo la biashara.
Rutageruka amesema, dagaa wa Zanzibar ni bidhaa nzuri na kwamba, wafanyabiashara kutoka nchi jirani wanakwenda kuzinunua.
“Kwa hiyo kuna eneo maalumu ambalo linapokea dagaa kutoka baharini lakini tunataka tuangalie namna gani ya kupata wawekezaji kuweza kuwekeza katika miundombinu mizuri zaidi ziweze kukaushwa vizuri zaidi, ziweze kuhifadhiwa vizuri na baadaye zikienda kwenye soko la nje ziende zikiwa tayari zimeongezewa thamani, wazifungashe vizuri ziende moja kwa moja ikiwezekana kwenye supermarket (maduka makubwa)”amesema.

No comments