Header Ads

Watoto milioni 2 wasajiliwa


Mpango huo upo chini ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ambao unaendeshwa kupitia Mkakati wa Kusajili Matukio Muhimu kwa Binadamu na Takwimu (CRVS).
Tangu mpango huo ulipoanza, unaendelea kutekelezwa katika mikoa 11 ambayo ni Mwanza, Mbeya, Iringa, Songwe, Njombe, Mtwara, Lindi, Geita, Shinyanga, Mara na Simiyu.
“Tathmini ya ujumla inaonesha Mpango wa Usajili wa Watoto umefanikiwa sana kwani mpaka kufikia sasa RITA na wadau wengine wamepata mafanikio makubwa katika mpango huu kwani zaidi ya watoto 2,324,349 wamesajiliwa kupitia mpango huu na inategemewa watoto takribani 400,000 zaidi kusajiliwa katika mikoa ya Mara na Simiyu ambapo kampeni ya kuondoa bakaa imezinduliwa wiki hii,” ilieleza taarifa ya RITA.
RITA imeeleza kuwa hayo ni mafanikio makubwa katika mpango huo ambao ulianza mwaka 2013 na kuenda kwa kasi zaidi kuanzia mwaka 2016 ambapo mikoa minane iliingia katika utekelezaji hadi kufikia sasa. Lengo la RITA ni kusajili watoto wote walio chini ya miaka mitano Tanzania Bara, na kwa mujibu wa Meneja Masoko na Mawasiliano wa Rita, Josephat Kimaro, usajili katika mikoa hiyo umekuwa na mafanikio makubwa.
Akielezea kuhusu usajili unaoendelea katika mikoa ya Mara na Simiyu, Kimaro alisema usajili unaendelea vizuri na kwa kipindi cha siku nane tangu kuanza usajili, zaidi ya watoto 277,000 wamesajiliwa katika mikoa hiyo miwili ambayo ni asilimia 37.8 ya lengo.
“Mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa na hii inaonesha wananchi wametambua umuhimu wa kuwa na cheti cha kuzaliwa,” alisema Kimaro.
Aliongeza maandalizi yameshaanza kwa ajili ya kuanza utekelezaji katika mikoa mingine zaidi ya Kigoma na Kagera hivyo kuwataka wananchi kuanza kujiandaa kuwasajili watoto ili wapate vyeti vya kuzaliwa.
RITA inatekeleza mkakati huo kwa kushirikiana na wadau wengine ambao ni Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto Duniani (UNICEF), Serikali ya Canada kupitia Shirika Idara ya Mambo ya Nje, Biashara na Maendeleo (DFATD), Kampuni ya Simu za Mkononi ya Tigo.
Mpango huo umeongeza uwezo wa RITA kuwa na takwimu kwani simu za kiganjani hutumika katika kuchukua na kutuma taarifa kwenda katika kanzidata ya wakala hivyo kusaidia utunzaji na upatikanaji wa kumbukumbu.
Kabla ya hapo, ilibidi kusubiri nakala ngumu kusafirishwa kutoka kila wilaya kwenda makao makuu ambapo zimekuwa hazifiki kwa wakati na nyingine kuharibika au kupotea.
Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Emmy Hudson alieleza kwamba mpango wa usajili wa watoto ni endelevu na siyo kampeni kama ilivyozoeleka na kwamba vituo vinavyosajili kwa sasa ni vya kudumu hata baada ya kumaliza bakaa la watoto wasio na vyeti vya kuzaliwa.
Pamoja na umuhimu wa cheti cha kuzaliwa bado wananchi wengi hawana vyeti vya kuzaliwa nchini. Kwa mujibu wa Takwimu za watu na makazi ya mwaka 2012 ni asilimia 13.4 tu ndiyo walio na vyeti vya kuzaliwa na zipo sababu nyingi za kimfumo wa usajili na kihistoria zilizosababisha hali hii.

No comments