WATU saba wamefikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera mjini Bukoba, kutokana na kupigwa na radi
WATU saba wamefikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera mjini Bukoba, kutokana na kupigwa na radi iliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo. Watu hao ni walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi Kyakairabwa iliyopo Kata ya Nyanga, Manispaa ya Bukoba.
Akithibitisha kupokelewa kwa watu hao waliopigwa na radi, Katibu wa hospitali hiyo, Kiiza Kilwanila alikiri kuwapokea majeruhi hao na kwamba wawili kati yao ni walimu na watano ni wanafunzi.
Kilwanila amesema majeruhi wawili walifikishwa hospitalini hapo wakiwa wamepoteza fahamu na baada ya kupatiwa huduma walirejea katika hali zao.
“Nitoe tahadhari kwa jamii katika kipindi hiki cha mvua watu waepuke kukaa chini ya miti kwa sababu mara nyingi radi huwa inatafutia sehemu ya kushukia kwenye ardhi pamoja na kuepuka matumizi ya vifaa vinavyotumia nishati ya umeme kama simu,” amesema.
Mwalimu wa zamu wa shule hiyo ya Kyakailabwa aliyekuwa mwangalizi wa majeruhi hao, Zainabu Jonathan amesema ilikuwa saa 2:45 asubuhi ghafla walisikia mngurumo mkubwa ulioambatana na radi na muda mfupi walisikia kelele za wanafunzi zikitokea.
Ameongeza kuwa baada ya kufika madarasani, walikuta wanafunzi wakiwa wameangukiana huku baadhi yao wakiwa wamepoteza fahamu, ndipo walipoanza kutumia magari ya walimu kuwapeleka katika hospitali hiyo.
Mwanafunzi Aneth David alisema walikuwa darasani wakifanya usafi wa darasa ndipo radi ilipopiga, akachuchumaa chini na kusikia kitu kikimkata tumboni na kuishiwa nguvu huku Nadhifa Majidi akisema walikuwa darasani wakijifunza, ndipo radi iliponyanyua dawati na kuwapiga hali iliyosababisha majeraha miguuni.
Diwani wa Kata ya Nyanga kupitia CCM, Deusdeth Mtakyawa alisema hilo siyo tukio la kwanza kutokea katika Mtaa wa Kyakairabwa kwani kwa historia ya eneo hilo watu watano wameshapoteza maisha kutokana na radi.
Rachel Rwegasira anayeishi jirani na eneo la tukio, alishauri serikali ione umuhimu wa kuweka mtego mpya wa radi katika shule hiyo kwa sababu uliopo unaonekana kuchoka na kuwa mdogo. Radi hiyo imesababisha taharuki na mshutuko kwa zaidi ya wanafunzi 60 wa shule hiyo.
Post a Comment