Header Ads

TRA yakamata tani 5 sukari


MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoani Tanga, imekamata majahazi manne yenye bidhaa mbalimbali katika Kijiji cha Kigombe wilayani Muheza kwa kupitia njia ya magendo zikitokea visiwani Zanzibar.
Akizungumza hivi karibuni baada ya kukamata majahazi hayo, Meneja wa Forodha wa TRA mkoani Tanga, Edward Ndupa alisema bidhaa zilizokamatwa ni tani tano za sukari, vitenge, khanga na mafuta ya kula madumu 470 ya lita 20 kila moja.
"Tumefanikiwa kukamata majahazi manne yakiwa na tani 5 za sukari, vitenge, khanga pamoja na mafuta ya kula madumu 470 ambapo thamani ya bidhaa zote hizo ni takribani Sh milioni 35," alisema Ndupa.
Ndupa alieleza kuwa, mpaka sasa wafanyabiashara wenye bidhaa hizo hawajafahamika, hivyo mamlaka hiyo inafanya utaratibu wa kuzitaifisha moja kwa moja bidhaa hizo.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Edward Bukombe aliwataka wafanyabiashara wote wanaojihusisha na biashara za magendo kuacha mara moja vitendo hivyo.
Aliongeza kuwa, jeshi hilo litaendelea kushirikiana na TRA, kuwakamata wote wanaosafirisha bidhaa kupitia njia sizizo rasmi.
"Natoa mwito kwa wafanyabiashara wote wanaokwepa kulipa kodi na kupitisha bidhaa zao katika njia za magendo kuacha mara moja tabia hiyo.
“Sisi kama Jeshi la Polisi, tumejipanga vizuri na tutaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania kuwabaini na kuwakamata wafanyabiashara wanaokiuka sharia, ikiwa ni pamoja na kukamata bidhaa husika," alisisitiza Bukombe.
Kamanda huyo aliwahimiza wafanyabiashara, kufuata sheria, kanuni na taratibu ili waweze kufanya biashara zao, bila kubughudhiwa na hatimaye waweze kujiingizia kipato kilicho halali.

No comments