Header Ads

amezindua ujenzi wa reli ya juu ya kisasa (SGR) yenye kilometa mbili itakayojengwa Mkoa wa Dar es Salaam kuanzia Stesheni hadi Buguruni





WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na M a w a s i l i a n o , Profesa Makame Mbarawa amezindua ujenzi wa reli ya juu ya kisasa (SGR) yenye kilometa mbili itakayojengwa Mkoa wa Dar es Salaam kuanzia Stesheni hadi Buguruni.
Aidha amewataka wakazi wa mkoa huo waliojenga pembezoni mwa reli kuhama kabla ya kubomolewa makazi yao. Akifafanua zaidi alisema kuwa reli hiyo ya juu inalenga kuwezesha treni kuendelea na safari yake bila kusababisha msongamano wa magari.Akizungumza wakati wa kuzindua ujenzi huo jana maeneo ya Shaurimoyo, jijini humo, Profesa Mbarawa alisema kuwa watu wengi wamekuwa wakilalamika kuwa hakuna ujenzi unaoendelea wa reli hiyo lakini wameamua kuwa na timu tatu za wakandarasi ambazo mojawapo itafanya kazi Dar es Salaam.
“Tumenzisha ujenzi wa reli ya kisasa kwa kipande hiki cha Dar es Salaam ambacho tunategemea hadi ifikapo Julai mwaka 2019 kitakwisha kwani kuna changamoto nyingi sana,” alisema Profesa Mbarawa. Alisema pia katika awamu ya kwanza ya mradi huo wakandarasi watakuwa Msoga, Ngerengere na Dar es Salaam na kwamba awamu ya pili itakuwa ya kuanzia Morogoro hadi Makutupora.
Alisisitiza kuwa miradi hiyo itagharimu Sh trilioni 7.6, hivyo aliwataka wakandarasi na mshauri wa mradi kuhakikisha wanasimamia ipasavyo ujenzi huo ili ukamilike kwa muda uliopangwa. Profesa Mbarawa alisema wanatarajia hadi ifikapo mwaka 2020 treni hiyo ya kisasa itazinduliwa kwa kuwa wanaamini wakandarasi wana utaalamu wa kutosha hivyo watapata reli yenye viwango vinavyotakiwa.
“Wakazi wa mkoa huu tunawaomba mtoe ushirikiano kwa wakandarasi kwa kuhama maeneo mliyojenga ambayo yapo pembezoni mwa reli bila kusubiri kubomolewa. Tunalenga kupata treni ya kisasa itakayoweza kutumika kwa miaka 100,” aliongeza. Katibu Mkuu wa Sekta ya Uchukuzi, Leonard Chamuhilo alisema kuwa mradi huo utaboresha mji huo, hivyo wanatarajia ushirikiano kutoka kwa wananchi ili ujenzi uweze kukamilika kwa wakati na kuongeza kuwa reli hiyo itakuwa na mapambo mbalimbali ambayo yataufanya mkoa huo kuwa na mwonekano wa tofauti.
Naye, Mwenyekiti wa bodi ya Shirika la Reli Tazania (TRC), Profesa John Kondoro alisema kuwa watahakikisha kuwa mradi huo unasimamiwa vyema ili kuleta maendeleo kwa taifa kwani ni fedha za kodi za wananchi zinatumika. Alieleza kuwa serikali imefanya uwekezaji mkubwa ambao ni lazima waone matunda ya mradi huo kwa malengo ya kuongeza pato la Taifa.

No comments