Header Ads

RAIS John Magufuli amewahakikishia Watanzania


Rais John Magufuli

RAIS John Magufuli amewahakikishia Watanzania kuwa  chini ya uongozi wake, serikali itaendelea kuboresha maisha ya wananchi wote kwa kuleta maendeleo ya aina mbalimbali, huku akiwataka kuilinda amani katika kuifi kia azma hiyo.
Akifungua Barabara ya Uyovu-Bwanga, wilayani Bariadi mkoani Geita yenye urefu wa kilomita 45, Rais Magufuli alisema ‘’kupanga ni kuchagua hivyo ni lazima kama Taifa tupange mambo mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya watanzania wenyewe”.
Alisema amani iliyopo nchini ni kichocheo tosha cha kuendeleza jitihada za serikali kutafuta maendeleo yanayohitajika na Watanzania, na hivyo hakuna sababu yoyote ya wananchi kudanganyika ili kuivuruga, ili kufikia malengo yaliyowekwa na serikali. Rais Magufuli alisema umoja na amani vilivyopo Tanzania ndivyo vitu pekee vitakavyoleta maendeleo ya taifa huku akieleza kuwa ndiyo jambo lililohubiriwa na mitume, hivyo ni vyema wananchi wakaacha kudanganyika ili kuivuruga na kuwa kama baadhi ya nchi majirani zetu.
“Naomba niwahakikishie kuwa nitaendelea kuisimamia amani iliyopo kwa nguvu zangu zote, viongozi wa dini, vijana pamoja na akinamama wote mna wajibu wa kuilinda msifikiri kwamba hii hali ya amani tuliyonayo watu wa mataifa mengine wanaifurahia,” alisema Magufuli. Alisema kwa sasa mambo yanayofanywa na Tanzania yakiwemo ya ujenzi wa reli ya kisasa, udhibiti madini, ujenzi wa barabara na mengineyo ni makubwa kiasi cha kusababisha watu wa mataifa hayo kuwa na chuki na Taifa hili, hatua aliyowataka wananchi kuwa kitu kimoja.
Aidha Rais Magufuli pia aliwaonya watendaji mbalimbali wanaoendelea kutoza ushuru wa mazao kwa wananchi wa kipato cha chini, hususani wale wanaouza ili kupata kiasi kidogo cha fedha kwa ajili ya kuendesha maisha yao, akisema kuwa suala hilo ni sheria hivyo hakuna mtu wa kuipinga. “Ushuru, ushuru, ushuru ni ugonjwa, huwezi kuwa na gunia moja halafu ulilipie ushuru, mzigo haujafika hata tani moja unamtoza mtu, utaratibu ni gunia ishirini na kuendelea, sitopenda kuona watu wa kipato cha chini wanyanyasike,” alisema Rais Magufuli.
Alisema maendeleo ya taifa hili kwa kiasi fulani yamechelewa hivyo ni vyema watanzania wakawa wamoja ili kufika mahali tulipopaswa kuwepo, huku akiipongeza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa jitihada inazozifanya katika maendeleo ya ujenzi wa barabara nchini. Aidha Rais Magufuli amewataka wananchi wa wilaya hiyo ya Bukombe kuwa wavumilivu wakati serikali inaendelea kushughulikia kilio chao cha kupatiwa ardhi kutoka hifadhi za Taifa kwa ajili ya kufanya shughuli za kilimo na ufugaji kama walivyoomba.
“Nafahamu kuwa asilimia 60 ya wilaya hii ya Bukombe ni eneo la pori, mliache tulifanyie kazi, wataalamu mbalimbali wakiwemo wa maliasili watakaa na kuzungumza ili kuona namna gani watalifanyia kazi,” alisema Magufuli. Aidha mbali na barabara hiyo, Rais Magufuli akiwa wilayani Kahama, pia alizindua barabara nyingine na kuwaelekeza viongozi wa Wizara ya Madini pamoja na mkoa, kuwalinda wachimbaji wadogo kulingana na sheria zinavyoeleza.
Alisema ili kuhakikisha uchimbaji unaofanywa na wachimbaji wadogo unakuwa wenye tija, serikali tayari imetenga maeneo matano ya mfano, kwa ajili ya wachimbaji hao yatakayowawezesha kufanya shughuli zao bila usumbufu wowote.
Rais Magufuli alisema nia ya serikali yake anayoiongoza ni kuona kila mwananchi anapata maendeleo huku akiwataka wananchi kuwauliza yeye na wabunge wa CCM kuwa wamefanya nini katika kipindi walichowaongoza. Aidha aliwaambia wananchi hao wa Kahama kuwa, ujenzi wa reli ya kisasa unaofanywa na serikali kuanzia Dar es Salaam hadi Rwanda, unatarajia kuinua uchumi wa wananchi hao na Tanzania kwa ujumla huku akiwataka kuchapa kazi kwa lengo la kujiletea maendeleo.

No comments