Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka kuwepo uchunguzi
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka kuwepo uchunguzi huru na wenye uwazi kuhusu mauaji ya waandamanaji 16 wa Kipalestina, waliouawa na wanajeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza Ijumaa, 30.03.2018.
Usiku wa Ijumaa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilifanya kikao cha dharura mjini New York, kufuatia ombi la Kuwait, lakini hakuna tangazo la pamoja lililoafikiwa kuhusu ghasia zilizojitokeza Ukanda wa Gaza. Makabiliano haya kati ya jeshi la Israel na Wapalestina ndio mabaya zaidi kutokea tangu vita vya mwaka 2014.
''Kuna wasiwasi kwamba hali hii inaweza kuzorota zaidi mnamo siku chache zijazo'', amesema Taye-Brook Zerihoun, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, na kuongeza kuwa umoja huo unataka pande husika zijizuie. Msemaji huyo vile vile amesema Umoja wa Mataifa uko tayari kuzipa msukumo mpya juhudi za mazungumzo kati ya Israel na Wapalestina.
Ufaransa pia imeonya kuhusu uwezekano wa kuzuka kwa mzozo mpya katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa kimabavu na Israel.
Mamia wajeruhiwa
Wizara ya afya katika Ukanda wa Gaza imesema kwamba pamoja na watu 16 waliouawa, wengine 1,400 walikuwa wamejeruhiwa, wakiwemo 750 wenye majeraha ya risasi za moto. Waliosaria walijeruhiwa kwa risasi za mpira.
Ni kwa sababu hiyo kwamba mabalozi wa nchi muhimu katika Baraza la Umoja wa Mataifa waliwakilishwa na wasaidizi wao, na hakuna tangazo lililoafikiwa katika kikao hicho.Marekani ambayo ni mshirika mkubwa wa Israel pamoja na Uingereza, zimesema zimesikitika kwamba kikao hicho kimefanyika wakati mbaya, sambamba na siku kuu muhimu ya dini ya Kiyahudi, hali iliyoufanya ujumbe wa Israel katika Umoja wa Mataifa usihudhurie kikao hicho.
Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa Riyad Mansour amesema amesikitishwa kwamba hakuna tangazo lililotolewa kulaani kile alichokiita, ''mauaji yenye chuki dhidi ya waandamanaji wa amani'', wala wito wowote wa kuwalinda raia wa Kipalestina.
Israel yasema Wapalestina wanaeneza uongo
Israel, kupitia ujumbe wa maandishi uliotumwa na ubalozi wake katika Umoja wa Mataifa, imewashutumu wapalestina kutumia muda ambapo Wayahudi kote duniani wanasherehekea siku muhimu ya Pasaka, ''kueneza uongo dhidi ya Israel''.
Wanajeshi wa Israel wamewafyatulia risasi waandamanaji wa kipalestina waliosogelea mpaka wake ambao umejengewa ukuta imara, na kwa kutumia vifaru walivishambulia vituo vitatu vya chama cha Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Wapalestina wameishutumu Israel kutumia nguvu za ziada katika kuyakandamiza maandamano. Kwa upande wake Israel imeyataja maandamano hayo kama njama ya chama cha Hamas kutaka kufanya mashambulizi ndani ya Israel.
Post a Comment