RAIS John Magufuli ametaka makubaliano yaliyofikiwa juu ya ushirikiano kati ya Tanzania na Israel
RAIS John Magufuli ametaka makubaliano yaliyofikiwa juu ya ushirikiano kati ya Tanzania na Israel katika maeneo mbalimbali yakiwemo ulinzi na usalama, mafunzo na masuala ya kiuchumi yatiwe saini haraka ili utekelezaji uanze mara moja.
Aliyasema hayo Ikulu Dar es Salaam jana baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa Israel, Avigdor Lieberman. Mazungumzo hayo yaliyofanyika jana yalihudhuriwa pia na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Ali Mwinyi, Balozi wa Israel nchini Noah Gal Gendler, viongozi wakuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Polisi.
Katika mazungumzo hayo, Rais Magufuli alimshukuru Lieberman kwa kuitembelea Tanzania na alimhakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ina dhamira ya dhati ya kuukuza zaidi na kuuimarisha uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Israel. Alitaka makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Israel katika maeneo mbalimbali yakiwemo ulinzi na usalama, mafunzo na masuala ya kiuchumi yatiwe saini Aidha, Rais Magufuli amemuomba Lieberman kumfikishia ujumbe Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu wa kumualika kutembelea Tanzania na pia kuanzisha ofisi ya ubalozi nchini badala ya kutumia ofisi za ubalozi zilizopo Nairobi nchini Kenya.
Kwa upande wake, Lieberman alimshukuru Rais Magufuli kwa kumkaribisha na kufanya naye mazungumzo na pia amemhakikishia kuwa Israel imejipanga kuongeza uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania katika maeneo yote ya makubaliano pamoja na kusaidia kilimo na usindikaji wa chakula. Juzi serikali ya Israel iliahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ili kuongeza utoaji wa huduma bora za matibabu kwa watoto wenye matatizo ya moyo nchini.
Ahadi hiyo ilitolewa na Waziri Lieberman alipotembelea JKCI kutathimini ushirikiano uliopo kati ya taasisi hiyo na taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto ya nchini Israel. Waziri Lieberman alipongeza mafanikio ambayo JKCI imeyapata katika utoaji wa huduma ya matibabu ya moyo na kuahidi kuendelea kushirikiana zaidi ili wananchi wenye matatizo ya moyo waweze kupata huduma bora.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu aliishukuru serikali ya Israel kwa mchango mkubwa wanaoutoa wa kuimarisha huduma ya matibabu ya kibingwa katika magonjwa ya moyo. Naye Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi alisema kadri madaktari wapatapo mafunzo zaidi ndivyo wanavyofanya upasuaji mara nyingi zaidi.
Post a Comment