kuharakisha ajira za kuwazika watu wasiokuwa na ndugu jijini humo
HALMASHAURI ya jiji la Dar es Salaam, imewataka wakurugenzi wa halmashauri za manispaa kuharakisha ajira za kuwazika watu wasiokuwa na ndugu jijini humo.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Meya wa Jiji hilo, Isaya Mwita, wakati akitoa taarifa kwa kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya pili ya mwaka.
Mwita amesema halmashauri zote zinatakiwa kulifanyia haraka suala la ajira hizo ili kusaidia shughuli za maziko kwa watu wasio na ndugu katika jiji hilo.
Amesema mpaka sasa Halmashauri ambayo imetekeleza agizo hilo ni Manispaa ya Kinondoni pekee, hivyo amezitaka halmashauri zilizobakia ikiwemo Ubungo, Kigamboni, Temeke na Ilala kujitahidi kutekeleza agizo hilo.
"Halmashauri ya Jiji tulipewa maagizo ya kuhakikisha tunazika miili ya watu waliofariki na kukosa ndugu, kawaida miili hiyo huichukua kwenda kuizika baada ya kukaa hospitali siku 21, na Jiji hutoa gari, dawa, sanda kwa marehemu huku halmashauri zingine zikihitajika kutoa watu wa kuwazika,” alisema Mwita.
Amesema, kila halmashauri inatakiwa kutoa watu wawili tu kwa ajili ya kazi hiyo hivyo ni vyema kuharakisha kufanya shughuli hiyo.
"Niwatake wakurugenzi wote wa halmashauri jitahidini kulifanyia kazi suala hilo ili kuziwezesha halmashauri zetu kupiga hatua kimaendeleo siyo kuzungumzia suala hili mara kwa mara," amesema.
Post a Comment