Header Ads

India yatuma waraka kwa Facebook

Symbolbild Facebook und Indien (picture-alliance/NurPhoto/N. Kachroo)

Serikali ya India imetuma waraka  kwa Facebook ikitaka kujua iwapo kampuni ya Uingereza ya Cambridge Analytica ilitumia data za wapigaji kura wa taifa hilo na watumiaji wa Facebook kuwashawishi kwenye uchaguzi mkuu. 
Waraka mwengine kama huo ulitumwa juma lililopita kwa kampuni ya Cambridge Analytica baada ya taarifa kwenye vyombo vya habari kudai kwamba, ilitumia data za raia wa India na kuathiri matokeo ya uchaguzi.
Serikali ya India imeweka tarehe 7 Aprili kuwa mwisho wa kampuni ya Cambridge Analytica kujibu waraka wake.
Facebook inakabiliwa na tuhuma baada ya ripoti kwamba kampuni hiyo ya Uingereza ilipata data ya mamilioni ya watu kwa njia haramu kutoka kwa watumiaji wa Facebook ili kuathiri matokeo ya uchaguzi.
India yataka Facebook kujibu ifikapo tarehe 7, Aprili
Kwenye taarifa yake siku ya Jumatano, Wizara ya Habari, Elektroniki na Teknolojia nchini India ilisema kuwa Facebook ina watumiaji wengi nchini humo na ilitaka kujua iwapo, ni hatua zipi inazochukua kuhakikisha usalama na siri ya watumiaji wake wengi ili data zao zisiweze kutumiwa vibaya na mtu mwengine.
Chama tawala cha Bharatiya Janata na kile cha upinzani vimeshutumiana kwa kutumia huduma za kampuni hiyo ya Uingereza lakini vikakanusha uhusiano wowote nayo.

Wataalamu wa masuala ya dijitali wanasema sheria za udhibiti nchini humo zina mapungufu makubwa.Inadaiwa kuwa kampuni ya Cambridge Analytica ilitumia bila ya ruhusa data za watumiaji wa Facebook zinazohusiana na data kwenye mashine za kupigia kura, suala ambalo limeibua mjadala kuhusu faragha kwenye matumizi ya vyombo vya kidijitali.

Waraka wa serikali ya India ulitaka kujua, "iwapo Facebook imewahi kuhusika kuathiri mchakato wowote wa uchaguzi nchini humo."
Wakati huo huo, Facebook siku ya Jumatano ilizindua mkakati mpya wa kuzima madai dhidi yake ya kudukua data za watu binafsi, kwa kuweka kitufe cha kibinafsi ambacho kitamuwezesha mtumiaji kuwa na udhibiti mkubwa wa habari au maelezo yake.
Mkakati huo mpya unajiri baada ya mtandao huo mkubwa wa kijamii kukosolewa baada ya kufichuliwa kuwa data za mamilioni ya watumiaji wake zilitumiwa na kampuni ya Uingereza inayohusishwa na kampeini za rais wa Marekani Donald Trump mwaka 2016.
Kampuni ya Facebook imekiri kuwa inahitaji kufanya mengi ili kuwafahamisha watu lakini imesema kuwa mabadiliko yako njiani.
Afisa mkuu wa masuala ya faragha wa kampuni hiyo Erin Egan na naibu mwanasheria wake, Ashlie Beringer, wamesema hayo kwenye taarifa ya blogu.



chanzo dw

No comments