watoto wadogo kubemenda,
KUATHIRIKA kiafya kwa baadhi ya watoto wadogo, mama anapopata ujauzito maarufu kama kubemenda, hakutokani na maziwa ya mama kuharibika anapopata ujauzito, bali huduma duni anazopata mtoto,” wamesema wataalamu.
Mmoja wa wataalamu hao ni Bingwa wa Watoto katika Hospitali ya Polisi ya Kilwa Road Dar es Salaam, Dk Nuru Letara; Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi ambaye pia ni Mratibu wa Uzazi Salama katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Koheleth Winani. Mwingine ni Mkuu wa Kitengo cha Lishe katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Scholastica James walisema hayo kwa nyakati tofauti walipozungumza na gazeti hili, mintarafu uhusiano uliopo baina ya mimba wakati wa kunyonyesha, na madhara ya kiafya kwa mtoto.
Scholastica anasema: “Hakuna uhusiano wa kifiziolojia wala kibaolojia kuhusu mama kupata ujauzito na kuharibika kwa maziwa ya mama, hivyo anayenyonyesha akipata mimba, aendelee kumnyonyesha mtoto huku naye akipata milo kamili, mapumziko, ushirikiano na kusaidiwa kisaikolojia.” Akaongeza: “Kitaalamu mama asipopata milo ya kutosha, na dhana iliyojengeka ya kuwa mama akipata ujauzito maziwa yanaharibika husababisha mtoto kuachishwa kunyonya na hivyo kumfanya mtoto yule hasa walio chini ya mwaka mmoja kutopata maziwa muhimu ya mama.”
Mtaalamu anasema, mama anapopata ujauzito akiwa na mtoto anayenyonya mahitaji ya mwili wa mama yanaongezeka hivyo anahitaji kupata milo ya ziada ili kupata virutubishi vya kutosha kukidhi mahitaji yake, mtoto aliyeko tumboni na mtoto anayenyonya. “Ikiwa mtoto atapata milo isiyo sahihi kwa mahitaji yake muhimu, hupata athari kiafya na ndio jamii huita kubemenda, kwani mtoto hupata utapiamlo mkali mfano unyafuzi au kwashakoo au vyote kwa pamoja na hivyo hudhoofu mwili na muda mwingine kusababisha kifo cha mtoto,” anasema Scholatica.
Naye Dk Nuru alisema: “Wanawake wengine wanapokuwa wananyonyesha, wanaweza kuweka nguvu zaidi kumhudumia mwanamume kuliko mtoto; mwingine anapata mimba inayomnyima nguvu ya kujihudumia mwenyewe na kumhudumia mtoto ipasavyo; yaani mtoto anapata huduma duni; wengine wanaacha hata kumnyonyesha mtoto kwa madai, eti maziwa yamechafuka jambo ambalo si kweli na ndiyo maana mtoto anaathirika.” Dk Winani yeye alisema ni uzushi wa kupindukia kusema makutano ya kimwili baina ya baba na mjamzito humwathiri na kumchafua mtoto tumboni na kwamba, sio kweli kuwa, mimba kwa mama anayenyosha husababisha maziwa kuchafuka na kumwathiri mtoto anayenyonya.
Post a Comment