Header Ads

Ndugulile amesema matatizo yanayoambatana na uzazi




NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile amesema matatizo yanayoambatana na uzazi, yanawafanya wanawake wawe katika hatari ya kupata magonjwa ya fi go ikilinganishwa na wanaume.
Dk Ndugulile alisema jana baada ya matembezi ya maadhimisho ya Siku ya Figo Duniani, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, ambayo kauli mbiu yake inasema ‘Figo na Afya ya Wanawake: Washirikishwe, Wathaminiwe na Wawezeshwe’. Alisema takwimu za Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), zinaonesha kuwa kati ya wajawazito watatu hadi watano kwa siku wanaopokewa hospitalini hapo, wanakuwa na matatizo hayo ya figo.
“Pamoja na matatizo ya kiafya yanayotokea wakati wa uzazi, yapo magonjwa yanayochangia matatizo ya figo ni pamoja na shinikizo la damu, ugonjwa wa kisukari, unene wa kupindukia, magonjwa ya saratani na magonjwa ya kuambukiza ikiwa ni pamoja na malaria,” alisema. Alisema, matatizo hayo kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na mtindo wa maisha ambayo yanaweza kuepukika kwa ulaji unaofaa, ufanyaji wa mazoezi pamoja na matumizi ya mbinu sahihi za kujikinga na magonjwa.
Dk Ndugulile alisema kauli mbiu ya siku ya figo mwaka huu inakumbusha kutambua mchango wa wanawake katika afya ya figo na kwa namna ya kipekee inataka tuwashirikishe, tutambue na kuwawezesha katika masuala yanayohusu afya ya figo. “Hii ni kaulimbiu muhimu inayotutaka kwanza kutambua wanawake wako katika hatari ya kupata magonjwa ya figo kuliko wanaume, hivyo katika mikakati yote ya kupambana na magonjwa haya tuwape kipaumbele akina mama… vile vile kaulimbiu hii inatukumbusha kuwa akina mama wana nafasi kubwa ya kuchangia katika kupambana na magonjwa ya figo ikiwemo kuamua ni aina gani ya chakula kitumike majumbani kwetu,” alisema.
Alisema mabadiliko ya mtindo wa maisha utasaidia kuokoa maisha na kuachana na gharama kubwa za matibabu. Kwa upande wa gharama za matibabu ya figo, Ndugulile alisema, figo haina mbadala ikiathirika ni lazima ibadilishwe au damu iwe inasafishwa kila wiki, ambapo ni kati ya Sh 250,000 mpaka Sh 500,000. “Ukienda mara nne kwa wiki gharama yake ni Sh 750,000 hadi Sh milioni mbili.
Hilo ni zoezi la kudumu na kwa mwaka inagharimu Sh milioni 37,” alisema. Alisema gharama ya kupandikiza figo nje ya nchi ni Sh milioni 75 hadi 77, kwa mgonjwa mmoja. Kwa hapa nchini kwa kuwa MNH imeshaanza kupandikiza figo gharama imepunguzwa mpaka Sh milioni 20.
Awali, Rais wa Chama cha Wataalamu wa Figo Tanzania (NESOT), Dk Onesmo Kisanga alisema Siku ya Figo Duniani ni kampeni ya kimataifa yenye lengo la kuongeza ufahamu unaohusu umuhimu wa kutunza figo ili kupunguza madhara yatokanayo na ugonjwa huo na pia kuhamasisha wananchi walinde figo zao dhidi ya magonjwa mbaimbali yanayoathiri figo.
Dk Kisanga alisema mtu mmoja kati ya 10 hupata tatizo la figo hivyo watu 195,000,000 duniani wamepata ugonjwa wa figo na kati yao 600,000 hupoteza maisha kila mwaka. Alisema wakina mama hupata magonjwa ya figo zaidi hasa wakati wakiwa wajawazito na wakati wa kujifungua, kwa mfano kupoteza damu nyingi na kifafa cha mimba na kuwa tafiti zilizofanyika Kaskazini Mashariki mwa Tanzania katika ngazi ya kaya mwaka 2014 zilionesha kuwa ugonjwa sugu wa figo unaathiri asilimia saba ya watanzania.

No comments