SERIKALI ya Japan kupitia ubalozi wake nchini imetoa misaada
SERIKALI ya Japan kupitia ubalozi wake nchini imetoa misaada mbalimbali inayolenga kuimarisha nyanja za elimu na biashara katika mikoa mitano.
Akizungumza jana Dar es Salaam baada ya kutiliana saini na wakurugenzi wa halmashauri ambazo zimenufaika na misaada hiyo, Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida aliweka bayana kuwa ubalozi huo umeguswa na changamoto zinazozikabili wilaya hizo.
Alitolea mfano wa mradi wa ugavi wa maji katika sekondari ya Kigwe iliyopo Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma ambayo haina huduma ya maji kwa muda mrefu.
Alisema Serikali ya Japan imeisaidia sekondari hiyo Sh milioni 240 kwa ajili ya kununua pampu mpya ya maji na kuweka mabomba ya kusambazia maji, matangi matano ya maji pamoja na vituo vya kuchotea maji vitano.
Alisema pia Japan imetoa Sh milioni 224 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya soko la samaki la Nyakarilo ambalo hakuna njia bora za utunzaji wa samaki na hivyo kulazimika samaki kuoza na kutupwa.
Aidha, alisema wamesaidia ujenzi wa hosteli ya wanafunzi katika sekondari iliyopo wilayani Moshi, Kilimanjaro ambako wanafunzi wanatembea kilometa 20 kwenda na kurudi shule, hivyo imetoa Sh milioni 173 za ujenzi wa hosteli na kununua samani.
Pia imetoa Sh milioni 219 kupanua Shule ya Msingi ya Kigoma iliyopo Manispaa ya Kigoma, ambayo itajenga madarasa 10 na vyoo huku Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya ikisaidiwa Sh milioni 135 kwa ajili ya ujenzi wa hosteli.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto pamoja na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya zilizonufaika na msaada huo.
Kwa upande wake, Dk Tulia alitoa mwito kuitaka Japan kuendelea kusaidia Tanzania hasa katika kuimarisha sekta binafsi ili kusaidia kupatikana kwa Tanzania ya viwanda kufikia mwaka 2025.
Post a Comment