Header Ads

Masogange kuhukumiwa Aprili 3


Image result for Agnes Gerald ‘Masogange’

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeshindwa kumsomea hukumu msanii Agnes Gerald ‘Masogange’ baada ya kuelezwa kuwa anaumwa, amewekewa dripu na hawezi kutembea.
Hukumu hiyo ilitakiwa kusomwa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya upande wa mashitaka na utetezi kufunga ushahidi wao.
Upande wa mashitaka uliokuwa ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula ulileta mashahidi watatu kutoa ushahidi dhidi ya Masogange na mshitakiwa huyo alijitetea mwenyewe.
Wakili wa Serikali, Adolf Mkini alidai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya hukumu ila mshitakiwa hayupo mahakamani hapo.
Baada ya kusema hayo, mdhamini wa Masogange aliiambia mahakama kuwa mshitakiwa huyo hakufika mahakamani kwa sababu anaumwa na kwamba amewekewa dripu, hivyo hawezi kutembea pamoja na kuwasilisha nakala za vyeti vya hospitali.
Hata hivyo, Mkini aliiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya hukumu. Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 3, mwaka huu. Masogange anatetewa na Mawakili, Reuben Simwanza na Nehemiah Nkoko.
Wakati akijitetea katika kesi hiyo ya kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin na Oxazepam, alidai hajawahi kutumia dawa hizo hata siku moja. Inadaiwa kuwa kati ya Februari 7 na 14, mwaka jana katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam alitumia dawa za kulevya aina ya Heroin (Diacety Imophine).

No comments