BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Anga (TCAACCC) limeitaka Kampuni ya Ndege ya Fastjet iwape fidia abiria wao walioahirishiwa safari zao bila kupewa taarifa.
BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Anga (TCAACCC) limeitaka Kampuni ya Ndege ya Fastjet iwape fidia abiria wao walioahirishiwa safari zao bila kupewa taarifa.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Debora Mligo alisema kampuni hiyo inalazimika kutoa fidia hiyo kwa mujibu wa sheria kutokana na madhara waliyoyapata abiria hao.
Mligo alisema kuanzia Jumatatu wiki hii baraza hilo lilipokea malalamiko mengi kutoka kwa watumiaji wa huduma za usafiri wa anga walioko maeneo ya Mwanza, Mbeya na Dar es Salaam kuhusu kuahirishwa kwa safari zao bila taarifa na lugha mbaya kutoka kwa wafanyakazi wa shirika holo.
Alisema malalamiko mengine ilikuwa ni kampuni hiyo kutowajali wateja wake baada ya kutokea mabadiliko hayo ya safari.
Alisema baada ya kupokea malalamiko, baraza lilichukua jukumu la kufuatilia suala hilo kwa ukaribu kw apande zote ikiwemo uongozi wa Fastjet ili kujua jitihada ambazo wamechukua kudhibiti hali hiyo.
"Uongozi wa Fastjet ulithibitisha kuahirishwa kwa safari zao mara kwa mara kwa kipindi tajwa kwa madai kuwa sababu hizo zilizokuwa nje ya uwezo wao na kwamba walikuwa wakifanya kila linalowezekana kurekebisha hali hiyo," ilisema taarifa.
Mligo alisema Fastjet pia ihakikishe mauzo yao ya tiketi yanayoendana na idadi ya ndege walizonazo na pia kuwe na utaratibu wa kutoa taarifa kwa abiria wake pale yanapotokea mabadiliko kwani taarifa ni haki ya msingi ya mtumiaji.
Katibu mtendaji huyo pia aliutaka uongozi wa Fastjet uwaelimishe wafanyakazi wake hasa walioko kwenye viwanja vya ndege kuwa na lugha nzuri na yenye staha kwa abiria. Pia alishauri uongozi uwajali abiria wake kwa kutoa tarifa sahihi bila kificho chochote kunapotokea mabadiliko ya safari.
Msemaji wa Fastjet, Lucy Mbogoro alipotafutwa alisema hawajasoma tangazo hilo la TCAA CCC na kwamba watazungumzia suala hilo la fidia baada ya kuwasiliana na mamlaka zilizotoa tamko hilo.
Alisema, mara baada ya ndege zao kuahirishwa, walitoa fursa mbili kwa abiria wao, moja ikiwa ni kuwarejeshea nauli abiria wao na kuwapa tiketi ya bure ndani ya miezi mitatu na wale ambao hawakukubali hilo waliwapa fursa ya kusafiri na ndege za kesho yake.
Alisema safari hizo ziliahirishwa kutokana na mabadiliko ya ndege, ambayo yamefanywa na kampuni hiyo na alisema usumbufu walioupata abiria waliuzungumzia juzi katika kikao kati yao na Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) na suala hilo la fidia halikuwepo na wala halikuzungumzwa.
Post a Comment