Header Ads

SERIKALI imeziagiza taasisi zote za umma kuhuisha taarifa katika tovuti zake

SERIKALI imeziagiza taasisi zote za umma kuhuisha taarifa katika tovuti zake, tovuti kuu ya serikali na kupokea na kujibu hoja za wananchi katika tovuti ya wananchi ili kuwapatia wananchi huduma bora.





Msemaji wa Serikali, Hassan Abbas ametoa agizo hilo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.
“Tovuti nyingi za serikali zina changamoto ya kutokuwa na taarifa mpya na zihakikishe maofisa mawasiliano na wataalamu wa Tehama kuanza mara moja kuhuisha tovuti hizo na taarifa muhimu zinazopaswa kuwepo katika tovuti hizo ili wananchi waweze kuziona, jambo ambalo litaleta uwazi,” alisema.
Abbas ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO).
Alisema kwa sasa huduma ya mitandao ni rahisi kuwafikia wananchi na kutoa taarifa kwenye mitandao ni sehemu ya uwajibikaji na sehemu ya uwazi kwa serikali hivyo mpaka mwisho wa mwezi huu ni lazima wawe wamehuisha na kuweka taarifa.
“Ikifika mwisho wa mwezi, tutafanya ukaguzi rasmi utekelezaji na ambao hawakutekeleza tutatangaza hatua za kuchukua kwa wale watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo,” alisema.
Amewataka maofisa mawasiliano wa taasisi hizo kuhuisha taarifa zao katika tovuti ya Serikali Kuu ambayo inawataka kutuma taarifa katika tovuti hiyo na mwisho wa mwezi huu watakaoshindwa kufanya hivyo watatangazwa hadharani na hatua nyingine za kiutawala zitachukuliwa.
Amesema, serikali kwa kuona umuhimu wa wananchi ilifungua tovuti ya wananchi, wanaoitumia kuuliza maswali na kutoa malalamiko, lakini baadhi ya maofisa hawajibu malalamiko yanayotolewa hivyo watalazimika kuweka hadharani majina ya wizara na taasisi zitakazoshindwa kutatua kero za mwananchi.
Alisema serikali ina taasisi 498, lakini mpaka sasa zenye tovuti ni 200, hivyo wameanza mkakati wa kuzisaidia halmashauri 93 kutengeneza tovuti na ametoa mwito kwa taasisi ambazo zinahitaji tovuti wawasiliane na Wakala ya Serikali Mtandao ambao wamepewa jukumu la kusimamia tovuti.
Ofisa Habari wa Wakala wa Serikali, Suzan Mshakangoto alisema kumekuwa na changamoto kubwa kwenye tovuti wengi hawafuati mpangilio na mwongozo wa tovuti, wengine wanatumia lugha ya Kiingereza na Kiswahili pamoja, lakini serikali iliagiza tovuti kuwa na lugha mbili kulingana na nchi ukiwa Tanzania ifunguke kwa Kiswahili na ukiwa nje ya nchi ifunguke kwa Kingereza.

No comments