Header Ads

Simba yalimwa faini ya mil 5, Mkude afutiwa kadi

Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeipiga faini ya shilingi milioni tano klabu ya Simba, kuiagiza ilipe gharama za uharibifu wa viti uliofanywa na washabiki wake katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya timu yake na Yanga




Jonas Mkude, baada ya kupewa kadi nyekundu katika mechi ya Yanga na Simba mwishoni mwa wiki iliyopita
Mechi hiyo ilichezwa Oktoba Mosi mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pia Kamati hiyo katika kikao chake kilichofanyika jana (Oktoba 4, 2016), imelaani kitendo hicho na kuionya klabu hiyo kuwa vitendo vya aina hiyo vikiendelea itakabiliwa na adhabu kali zaidi ikiwemo kucheza mechi bila washabiki.
Taarifa iliyotolewa leo na Afisa Habari wa TFF, Alfred Lucas imesema kuwa adhabu dhidi ya Simba imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 42(3) na 24(7) za Ligi Kuu.
Vilevile taarifa hiyo imesema kuwa kwa kuzingatia Kanuni ya 9(8) ya Ligi Kuu, Kamati imefuta adhabu ya kadi nyekundu iliyotolewa na mwamuzi wa mechi hiyo kwa Jonas Mkude wa timu ya Simba baada ya kuthibitika bila mashaka kuwa nahodha huyo hakustahili kadi hiyo.
Mbali ya ripoti ya Kamishna na kupitia tena mkanda wa mechi hiyo iliyoonyshwa 'live', Kamati inaendelea na uchunguzi wa jambo lingine kuhusu uchezeshaji wa mwamuzi wa mechi hiyo Martin Saanya, na wasaidizi wake Samwel Mpenzu na Ferdinand Chacha kabla ya kutangaza uamuzi wake.
Katika hatua nyingine, Lucas amesema kuwa Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Manara amepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa kuingia uwanjani baada ya mechi hiyo wakati yeye hakuwa miongoni mwa maafisa wa mechi waliotakiwa kuwepo katika eneo hilo.
Amesema adhabu dhidi ya Manara ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(10). Eneo husika ni kwa ajili ya wachezaji, mabenchi ya ufundi, waamuzi, madaktari, huduma ya kwanza, wapiga picha na maofisa wengine wa mechi.

No comments