Header Ads

BWENI LA SHULE YA SEKONDARI UFUNDI MTWARA LATEKETEA KWA MOTO


Bweni la wasichana wa shule ya sekondari ya Mtwara ufundi iliyoko katika Manispaa ya Mtwara Mikindani limeteketea kwa moto leo majira ya saa moja asubuhi.

Akizungumza katika eneo la tukio kamanda polisi Mkoani hapa Thobias Sedoyeka amesema kwamba majira ya saa moja katika shule ya sekondari ufundi kulitokea moto ambao ulianza kuwaka katika mabweni ya wasichana ambapo mpaka sasa chanzo hakijajulikana na kuongeza kuwa hakuna madhara yoyote yaliyotokea kwa binadamu na makadirio ya hasara ya thamani ya jengo na mali zilikuwemo  bado haijajulikana.
 
Naye mwalimu wa shule hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Nanyalika amesema kwamba alikuwepo eneo la tukio wakati bweni hilo la wasichana wa shule ya sekondari ya ufundi linaanza kuteketea ambapo kwa upande wake hajui chanzo cha moto huo hali ambayo imepelekea walimu ambao wanaishi ndani ya shule hiyo kuwa na hali ya sintofahamu kwa kuhofia usalama wao.
 
kwa upande wake mwalimu wa shule ya sekondari Sululu Sekondari iliyoko Mjini Masasi ambae yupo shuleni hapo kwa ajili ya kusahihisha mitihani ya kidato cha pili na alikuwa akitumia moja ya chumba cha bweni hilo amesema kwamba kipindi ambacho wapo katika maeneo yao ya kazi ndipo walipoona moshi unatokea kwenye bweni.
 
Naye mwalimu Masele Francis kutokea shule ya sekondari ya Namwombe iliyoko katika Halmashauri ya Masasi ameeleza kuwa kipindi ambacho anatoka bwenini aliona moshi mkubwa hali ambayo ilimpelekea kurudi ndani ili kuwapa wenzake taarifa.
 
Aidha  Afisa Habari wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Bi.Jamad Omary amewatoa hofu walimu pamoja na wanafunzi wa shule hiyo na kuwaomba kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu mbali na hayo amewataka wananchi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani kuwa na ushirikiano wa kutosha pindi kunapotokea tatizo kama hilo na si kuishia kutoa lawama.
 
Hata hivyo Kamanda amesema kwamba taarifa kamili kuhusiana na tukio hilo ikiwemo chanzo cha moto huo itatolewa baada ya taratibu zote kukamilika.


No comments