MAJAMNBAZI 103 MBARONI
POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imefanya msako katika maeneo ya Jiji na kuwakamata watuhumiwa sugu 103 wa makosa mbalimbali ya uhalifu, ikiwemo unyang’anyi wa kutumia nguvu.
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Simon Sirro alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika operesheni iliyofanyika kwa wiki moja kuanzia Desemba 2 mwaka huu katika maeneo mbalimbali kwa nyakati tofauti.
Aliyataja makosa hayo kuwa ni kuvunja nyumba usiku na kuiba; wizi kutoka maungoni; kucheza kamari; kubughudhi abiria; wizi wa magari; kutengeneza, kuuza na kunywa pombe haramu ya gongo; na uvutaji bangi.
Sirro alisema operesheni hiyo ni endelevu na kuwaomba raia wema kuendelea kutoa taarifa za uhakika za kuhusu uhalifu unaotendeka, uliotendeka na unaotarajiwa kutendeka.
Wakati huo huo, Sirro alisema Polisi kupitia kikosi chake cha usalama barabarani kimekamata makosa mbalimbali ya usalama barabarani kwa kipindi cha wiki moja kuanzia Desemba 2 kimeiingizia serikali mapato ya ndani ya Sh 451,590,000 katika mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema idadi ya magari yaliyokamatwa ni 13,496, pikipiki 1,296, daladala 5,713, magari mengine binafsi pamoja na malori 7,783 huku bodaboda waliofikishwa mahakamani kwa makosa ya kutovaa kofia ngumu na kupakia mishikaki ni wanne.
Alisema jumla ya makosa hayo yaliyokamatwa yalikuwa ni 15,053 na jumla ya fedha za tozo zilizopatikana ni 451,590,000 na kuwataka madereva kuwa makini katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka ili kuepuka ajali
Post a Comment