Header Ads

WAZEE wawili wameuawa Mkoa wa Rukwa



WAZEE wawili wameuawa, mmoja kwa kuchinjwa na mwingine kwa kupigwa rungu kisogoni mwa mwanawe wa kiume.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema mauaji hayo yalitokea Desemba 6, mwaka huu usiku wa manane katika Kijiji cha Kichangani.

Katika tukio la kwanza, mkazi wa Kijiji cha Kichangani kilichopo mwambao mwa Ziwa Tanganyika katika Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, Joseph Mpenda maarufu “Chondo” (70) alikufa baada ya kupigwa rungu kisogoni na mwanawe, Mussa Mpenda (32).

Kamanda Kyando alisema usiku huo wa tukio, mtuhumiwa alimvizia baba yake akiwa amelala nyumbani kwake ambapo chanzo cha mauaji hayo hakijajulikana huku uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Alisema mtuhumiwa alitoroka baada ya kufanya mauaji hayo na kujificha kusikojulikana.

Katika tukio jingine, mkazi wa kijiji cha Mwadui kilichopo katika Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga, Lises Magadula (65) amechinjwa baada ya kuvamiwa na watu wanne ambao hawafahamika. Aliuawa juzi saa tano usiku kijijini hapo.

Kamanda Kyando alisema katika tukio hilo, mwanamke Gindu Kashinye (50) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Mwadui alijeruhiwa shingoni na begani akiwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa iliyopo ambapo mjini Sumbawanga kwa matibabu huku hali yake ikiwa tete.




chanzo habari leo

No comments