Header Ads

Arsene Wenger: Marefa wanalindwa kama simba Uingereza

Arsene Wenger
Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amesema waamuzi nchini Uingereza wanalindwa kama simba kwenye kituo cha kuhifadhi wanyama, baada ya Arsenal kulazwa na Manchester City 2-1 Jumapili.
Wenger anasema maamuzi mabaya ya refa yaliigharimu klabu yake ushindi.
Arsenal walikuwa mbele kabla ya Leroy Sane kusawazisha, ingawa kanda za video zinaonyesha alikuwa ameotea kidogo.
Na David Silva alikuwa pia amejenga kibanda ardhi ya City wakati Raheem Sterling alipofunga bao la ushindi.
Hata hivyo si wazi iwapo alingilia uchezaji wa kipa Petr Cech.
"Ni vigumu kukubali (matokeo) katika mchezo wa aina hiyo," amesema Wenger.
"Lakini, inajulikana wazi, kwamba marefa wanalindwa sana kama simba kwenye kituo cha kuhifadhi wa nyama, kwa hivyo inatulazimu kukubali uamuzi wao."
Alipotakiwa kufafanua, Wenger alisema: "Nataka walindwe vyema, na nataka wahakikishiwe usalama wao, lakini iwapo wangekuwa wanafanya maamuzi sahihi, ingekuwa hata bora zaidi."
Aliongeza: "Ninaelewa kwamba City wanaonekana kuwa an furaha sana - Hata mimi ningefurahi - lakini nafikiri mabao hayo yalikuwa ya kuotea."
Gunners waliongoza ugenini Etihad kupitia bao la Theo Walcott mapema lakini City wakajikwamua kipindi cha pili.
Ushindi wao uliwawezesha kuwaruka Arsenal na kutua nambari ya pili kwenye jedwali, Arsenal nao wakashuka hadi nambari nne.
Wenger pia alilaumu mwamuzi Arsenal waliposhindwa na Everton Jumanne, hatua iliyomfanya meneja wa Everton Ronald Koeman kumcheka kwa kutilia shaka uamuzi wa refa Mark Clattenburg.
"Imekuwa wiki mbaya sana," alisema Wenger.
"La kusikitisha zaidi ni kwamba tulicheza vizuri mechi mbili lakini tukaondoka na alama sifuri na, tulikuwa tunaongoza mechi hizo mbili, tulipoteza michezo miwili."
Arsenal watakutana na West Brom siku ya Boxing Day (Desemba 26) na kisha wakutane na Crystal Palace siku ya Mwaka Mpya.


No comments